WANANCHI WA KATA YA RUSOLI WAHAMASIKA NA UJENZI WA MAABARA KWENYE SEKONDARI YA KIJIJINI MWAO

UPAUAJI wa  JENGO la MAABARA unaendelea kwenye Shule ya Sekondari Rusoli. Aliyevaa kofia kwenye picha ni Mhe Diwani Boaz Nyeula alipotembelea Maabara ya Sekondari ya Rusoli.

Na. Verediana Mgoma, Msaidizi wa Mbunge
Wananchi wa Jimbo la Musoma Vijijini wameendelea kuhamasika katika Ujenzi wa Maabara kwenye Shule za Sekondari za Kata zao.
Wakazi wa Kijiji cha Rusoli wameendelea KUJITOLEA kuweka NGUVU ZAO kwenye Sekondari ya Rusoli ili kukamilisha JENGO la MAABARA litakalotumika kujifunza MASOMO YA SAYANSI kwa VITENDO.
Sekondari hiyo imepata msaada wa VIFAA vya MAABARA kutoka kwa Ndugu Japhet Makongo mzaliwa wa Kijijini hapo na MDAU MKUBWA wa ustawi na maendeleo ya Sekondari ya Kijijini kwao Rusoli.
WANAFUNZI wa Sekondari ya Rusoli wamekuwa wakipata shida katika MASOMO YA SAYANSI ya VITENDO kwa kukosa vifaa vya maabara kwa muda mrefu hivyo kupatikana kwake kutaondoa adha waliyokuwa wakiipata Wanafunzi hao.
Bi.Tausi Juma ambaye ni Mkuu wa Shule ya Sekondari Rusoli alisema licha ya kupatikana kwa vifaa hivyo tatizo kubwa linalowakabili ni KUTOKUWEPO JENGO LA MAABARA na kupelekea VIFAA VYA MAABARA VILIVYOPATIKANA kuhifadhiwa DARASANI.
Wanafunzi na Walimu wamefurahia sana kuona UJENZI WA MAABARA umeanza shuleni hapo.
HALMASHAURI YA WILAYA YA MUSOMA IMETOA Tshs MILIONI 25 kwa ajili ya UEZEKAJI WA JENGO HILO na ukamilishaji wa chumba kimoja huku Shule ikiwa na changamoto ya ukamilishaji wa Vyumba vingine viwili vya Maabara vinavyohitaji Saruji Mifuko 400, madirisha na milango.
Wanakijiji, Wanafunzi na Walimu wa Sekondari WANAOMBA WAFADHILI wajitokeze kukamilisha ujenzi huu muhimu sana kwa MASOMO YA SAYANSI shuleni hapo.
Kwa upande wake, Mwalimu anayesimamia Maabara katika Shule hiyo, Mwalimu Joseph Kasili alisema uwepo wa Vifaa hivyo vya Maabara umetoa hamasa kubwa kwa WANAFUNZI  kupenda Masomo ya Sayansi.
Sekondari ya Rusoli inashukuru kupokea mara mbili VITABU VYA MASOMO YA SAYANSI kutoka kwa Mbunge Prof Sospeter Muhongo aliyeletewa vitabu hivyo kutoka USA na UK.
Diwani wa Kata hiyo Mhe Boaz Nyeula  amewashukuru ndugu, jamaa na marafiki wanaoendelea KUJITOLEA kwenye suala zima la maendeleo kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Profesa Sospeter Muhongo kuipa ELIMU kipaumbele na kuwaomba Wadau wengine mbalimbali kuwaunga mkono ili kukamilisha UJENZI wa MAABARA hapo shuleni.
Aidha, Diwani huyo ameishukuru Ofisi ya Mbunge kwa msaada wa Saruji Mifuko 70  iliyotolewa hapo Shuleni  na kutumika kukarabati Vyumba vya Madarasa huku lengo likiwa ni kujenga Mazingira bora ya Elimu.