SHULE YA SEKONDARI KASOMA KUJENGEWA MAABARA YA KISASA

Naibu Waziri wa Elimu William Ole Nasha (wa pili kulia) akiwa kwenye ukaguzi wa shule ya Sekondari Kasoma. Wengine kwenye picha ni Ibrahimondi Malima (wa kwanza kulia) ambaye ni Kaimu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma na Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney (wa pili kushoto).

Na. Fedson Masawa

NAIBU Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William  Ole Nasha ameahidi ujenzi wa maabara kubwa ya kisasa katika shule ya Sekondari Kasoma ikiwa ni hatua muhimu ya kutoa elimu bora kwa masomo ya sayansi nchini.

Ole Nasha alitoa ahadi hiyo wakati alipozungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari Kasoma katika ziara yake aliyoifanya kwenye Halmashauri ya Musoma ambapo alikagua miradi miwili; Lipa kulingana na matokeo (P4R) uliokuwa ukitekelezwa katika shule mbili za Musoma vijijini ambazo ni shule ya msingi Kamguruki iliyopo kata ya Nyakatende pamoja na shule ya sekondari Kasoma iliyopo kata ya Nyamrandirira.

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri huyo aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Kaimu Mwenyekiti wa Halmashauri na wakuu wa idara kutoka Halmashauri ya Musoma, ambapo alikiri kuridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo na kusema ni ishara ya matumizi mazuri ya fedha za serikali.

“Hongereni sana Musoma vijijini kwa kutumia vizuri fedha za serikali na wafadhili. Hii inatupa chachu ya kuendelea kusaidia miradi ya maendeleo alisema Naibu Waziri Ole Nasha.

Katika miradi hiyo miwili, mradi wa shule ya msingi Kamguruki uliotumia Shilingi milioni 112 umekamilika kwa kujengwa vyumba vinne vya madarasa, choo cha wanafunzi matundu 20, ofisi mbili za walimu, maktaba moja na ukarabati wa vyumba vya madarasa.

Katika shule ya sekondari Kasoma iliyopokea jumla ya Shilingi milioni 236, Naibu Waziri amejiridhisha na ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa, kazi ambayo imekamilika na ujenzi wa mabweni mawili yenye vyumba 24 kazi ambayo inaelekea mwishoni.

Hata hivyo, Naibu Waziri Ole Nasha alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof. Sospeter Muhongo kwa jitihada kubwa anazozifanya Jimboni mwake za kuboresha elimu hasa katika uchangiaji wa madawati katika shule zote za Musoma vijijini, ujenzi wa vyumba vya madarasa na usambazaji wa vitabu kwa shule zote za sekondari na msingi.

Kwa upande wao wanafunzi wa shule ya sekondari Kasoma wametoa shukrani zao kwa serikali kupitia kwa viongozi wao na kuahidi kufanya vizuri katika masomo yao hasa watakapopata maabara kwa ajili ya masomo ya Sayansi.

“Tunashukuru serikali na viongozi wetu kwa kuweka elimu kama kipaumbele cha maendeleo. Ujenzi wa maabara kwetu utatoa fursa kwetu kufanya vizuri zaidi hasa katika masomo ya sayansi” alishukuru Elizabeth Michael, mwanafunzi wa kidato cha nne.