MVUA KUBWA YASABABISHA MAAFA MUSOMA VIJIJINI

Msaidizi wa Mbunge James Francis akikabidhi mchango ikiwa ni rambi rambi kutoka ofisi ya mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini kwa familia ya ndugu waliopatwa na maafa kufuatia mvua kubwa iliyonyesha jana usiku.

Na. Verdiana Mgoma

MVUA kubwa iliyonyesha jana usiku imesababisha maafa makubwa ikiwemo vifo vya watu watatu wa familia moja waliopoteza maisha baada ya kuangukiwa na nyumba kwenye kijiji cha Bwai Kumsoma, Musoma vijijini.

Msemaji wa familia hiyo ambaye ni baba wa majeruhi Makukumbile Chrismas alisema, mvua hiyo kubwa ilianza kunyesha mnamo saa sita usiku huku mke na watoto wake wakiwa wamelala, ndipo walipoangukiwa ukuta wa nyumba na kupoteza maisha.

Makukumbile alisema, iliwachukua muda mrefu hadi majirani kujua kama mtoto wake na familia yake wamepatwa na tatizo hilo, ambapo mmoja wa marafiki wa mwanaye ndiye aliyegundua tatizo hilo alipokwenda kumfuata rafiki yake ili waende ziwani kuvua samaki ambapo alimkuta akiwa amelala huku akiomba msaada kwa majirani.

Kwa upande wake Mtendaji wa kata ya Bwai, Pendo Mwita alisema, kabla ya kupatwa na dhoruba hiyo, tayari nyumba ya Michael Makukumbile ilikuwa na nyufa ambazo wao hawakutambua mapema kama zingeleta madhara.

Aidha, mtendaji huyo alithibitisha vifo vya watu watatu ambao ni wanafamilia akiwemo mama anayeitwa Stella Magembe na watoto wawili Ester (3) na Chrismas (miezi saba) huku baba wa familia hiyo Michael Makukumbile akiendelea na matibabu katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) kutokana na majeraha aliyoyapata.

“Kuna rafiki wa majeruhi ambaye ni Baba wa familia hii, alikuwa akijishughulisha na uvuvi alimfuata waende ziwani alipofika nyumbani kwake akawa anasikia sauti za kuomba msaada, ndipo naye akatoa taarifa kwa majirani ili kumsaidia kumtoa majeruhi huyo” alisema Pendo.

Kutokana na tukio hilo, mtendaji huyo amewataka wananchi wa eneo hilo kufuata ushauri wanaopewa kuhusiana na ujenzi ulio bora kuliko kujenga bila kufuata utaratibu, huku akiahidi kushirikiana na viongozi wa eneo hilo kutoa elimu kupitia mikutano ya hadhara pamoja na makanisa.

Naye Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho Ibrahimu Kaale alimshukuru Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo kwa kuungana nao katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo, ambapo kupitia ofisi ya mbunge ametoa rambi rambi ili kuwafariji wahanga hao huku akiahidi kuwatembelea wote waliopatwa na tatizo hilo.