PROF. MUHONGO AZINDUA UJENZI WA KITUO CHA AFYA NYAMBONO

Mratibu wa mradi wa ujenzi wa kituo cha afya Nyambono Dkt. Majura Songo (kushoto) akisoma taarifa ya mradi huo. Kulia ni mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye hafla hiyo, akifuatilia kwa makini taarifa hiyo.

 Na Fedson Masawa

MBUNGE wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo amezindua ujenzi wa Kituo cha afya katika kijiji cha Nyambono kata ya Nyambono kwa kuweka jiwe la msingi.

Hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa jimbo la Musoma vijijini wakiwemo madiwani na wananchi wa kata ya Nyambono, imefanyika Disemba, 25, 2017 katika viwanja vya kituo cha afya Nyambono kinachojengwa kijijini hapo.

Awali akifungua hafla hiyo, Kaimu mwenyekiti wa kijiji cha Nyambono Sostenes Majura alisema, wananchi wa kijiji cha Nyambono wana hamasa kubwa ya kushiriki shughuli za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuchangia nguvu kazi na michango mbalimbali itakayokuwa inahitajika.

Majura alitumia hadhara hiyo kuwaomba viongozi mbalimbali na wananchi wenye moyo wa kujitolea waishio nje ya kijiji na kata ya Nyambono wawaunge mkono ili kufanikisha shughuli hizo za ujenzi wa kituo hicho ambacho kitakuwa na vyumba vya uangalizi maalum na vyumba vitatu vya madaktari.

Akisoma taarifa ya mpango na utekelezaji wa mradi huo wa ujenzi wa kituo hicho cha afya, mratibu wa mradi huo Dkt. Majura Songo ambaye pia ni mzawa katika kijiji cha Nyambono alisema, kijiji cha Nyambono kina watu zaidi ya 5,000 ambao wamekuwa wakipata huduma za matibabu katika zahanati ya kijiji cha Saragana ambayo nayo imeelemewa na wagonjwa.

Mratibu huyo aliendelea kusema, lengo la mradi huo ni kuwaondolea usumbufu wananchi wa Nyambono na umebuniwa na wananchi wenyewe kwa kushirikiana na wazawa wanaoishi nje ya kijiji cha Nyambono na kwa umoja na mshikamano huo, tayari wameungana na zoezi la uchangiaji limekwishaanza na fedha hizo zinachangwa moja kwa moja kwenye ofisi ya Mbunge zilizopo Saragana.

Dkt. Songo alisisitiza kuwa, mradi wa ujenzi wa kituo cha afya ni shirikishi ambapo unawahusisha wananchi wa kijiji cha Nyambono walioko ndani na nje ya kijiji, marafiki, viongozi wote wa Musoma vijijini na Halmashauri ya wilaya ya Musoma, huku wananchi  wanashiriki nguvu kazi kama vile kusomba mawe, mchanga na mafundi, wananchi waishio nje ya Nyambono wanashiriki kutoa michango ya saruji 350 ambayo tayari imepatikana mifuko 69 na zoezi bado linaendelea.

“Ndugu mgeni rasmi, mradi huu ni shirikishi ambapo unajumuisha wananchi walioko nje na ndani ya kijiji cha Nyambono, viongozi wa kata na kijiji pamoja na Halmashauri ya wilaya ya Musoma” alieleza Dkt. Songo.

Hata hivyo, kituo cha Nyambono kimekadiriwa kugharimu shilingi za kitanzania bilioni 2.2 na kitakuwa na jumla ya majengo 12 likiwemo jengo la OPD ambalo tayari ujenzi wake umeanza kutekelezwa, jengo la mama na mtoto na majengo mengine yote kulingana na muongozo kamili wa ujenzi unaostahili kwa mujibu wa taratibu.

Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo aliwashukuru wananchi wa kijiji cha Nyambono kwa kubuni mradi huo mzuri na ameahidi kuchangia shughuli nzima ya uezekaji wa majengo hayo mara tu yatakapokuwa yamekamilika ujenzi wake.

Akitoa shukrani zake kwa niaba ya wananchi wa kijiji na kata ya Nyambono, Mkoyongi Masatu amewashukuru viongozi wote na wananchi waliojitolea kuchangia michango yao ili kufanikisha ujenzi wa kituo hicho cha afya.

Aidha, Masatu alimshukuru Prof. Muhongo kwa kujitolea kuwaezekea majengo hayo na ameahidi ushirikiano mkubwa ili kufikia Juni 2018 ujenzi huo uwe umekamilika.

“Nitumie fursa hii muhimu kuwashukuru viongozi, Mbunge na wananchi kwa ujumla kwa jitihada zao na michango yao ili kuhakikisha kituo hiki kinakamilika katika muda muafaka. Nami naahidi kutoa ushirikiano mkubwa ili nisimuangushe wala kuupoteza mchango wa Mbunge na ifikapo Juni 2018 kituo kiwe kinaanza kazi” alishukuru na kusema Mkoyongi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi wa kijiji cha Nyambono wamesema, suala la kujenga kituo cha afya ni jitihada pekee za kuondoa usumbufu, kuleta maendeleo na kupunguza vifo vya mama na mtoto kwani huduma hiyo tayari itakuwa imesogea karibu na jamii hizo ukilinganisha na huduma ya awali inayopatikana katika kijiji cha Saragana na kata za jirani.

Hafla hiyo ya uwekaji wa jiwe la Msingi ilienda sambamba na sherehe za sikukuu ya Krismasi ambapo Prof. Muhongo aliungana na marafiki zake Dkt. Christa na Wolf kutoka Ujerumani walioungana na wananchi wa jimbo lake kuazimisha sikukuu hiyo kwa kushiriki chakula cha pamoja na wananchi wake.

Kabla ya kushiriki hafla za uwekaji wa jiwe la msingi, Prof Muhongo na marafiki wake walipata fursa ya kuhudhuria misa takatifu katika kanisa la Menonite lililopo kijiji cha Nyambono.