KIKAO CHA KWANZA CHA BARAZA LA MADIWANI CHAFANYIKA MURANGI

Wananchi waliohudhuria kikao cha madiwani (full council) kilichofanyika kwenye viwanja vya Murangi.

Na. Verdiana Mgoma

MADIWANI wa Musoma Vijijini wamekubaliana kuhamisha rasmi shughuli zake kwenye Makao Makuu ya Halmashauri hiyo yaliyopo kwenye kijiji cha Murangi.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Charles Magoma alisema, wameamua kuhamia rasmi nyumbani ambako ni Murangi na kuanzia sasa vikao vyote vitafanyika huko.

Magoma alisema, watahakikisha wanatafuta ofisi hata kama ni mbovu, lakini wataanza hivyo hivyo: “maana mwanzo huwa mgumu inabidi tukubaliane na kasi ya awamu ya tano”

Mkurungenzi wa Halmashauri ya Musoma Vijijini Flora Yongolo alisema, hilo ni tukio la kihistoria kwa Halmashauri hiyo kuchukua maamuzi ya kuhamia Murangi ambako ndipo kwenye makazi yao.

“Kwa historia kikao hiki kitafanyika wazi kwa wananchi ili wajue nia na madhumuni yetu ni kuhamia rasmi Murangi. Lengo letu siyo kuhamia Murangi tu, tunahitaji pia kujenga halmashauri yetu na kujitegemea kwa kuwa tumedhamiria kufanya hili, tutahitaji kupata msaada wa pesa kutoka serikalini tayari kwa kuanza ujenzi” alisema Yongolo.

Kwa upande wake diwani wa Kata ya Nyamrandirira, Ruteli Maregesi amewakaribisha madiwani hao kwenye kijiji cha Chumwi endapo kutakuwa na shida ya sehemu ya kufanyia vikao.

Diwani huyo ameshukuru kwa uamuzi huo waliochukua madiwani wenzake na kuungana kwa pamoja kufanikisha zoezi walilopigania kwa muda mrefu.

“Imefika tamati, tumefanikisha kurudi Murangi hili ni jambo la kheri kwetu na kwa wananchi wa jimbo la Musoma vijijini” alisema diwani Maregesi.

Naye Mkuu wa wilaya ya Musoma Dkt. Vicent Anney alisema, anaunga mkono maamuzi yaliyochukuliwa na Halmashauri ya Musoma vijijini ya kuhamishia makazi yake rasmi Murangi, jambo ambalo linaonesha nia ya kukubaliana na mabadiliko ya awamu tano.

“Hata Rais aliposema anahamia Dodoma watu hawakuamini, lakini na sisi pia tumejifunza kutoka kwa mkuu wetu kama ameweza kuhamia Dodoma, kwetu inakuwaje ngumu kuhamia Murangi?” alihoji Mkuu wa wilaya.

Mkuu wa Wilaya Dkt. Vicent Anney alisema, kwa kuonesha wamedhamiria kwa maamuzi hayo, ameahidi kutoa taarifa kwa ngazi za juu ili waweze kupata pesa kwa ajili ya ujenzi wa Halmashauri hiyo.

Hata hivyo, alisisitiza maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, hali ya chakula na matumizi ya fedha kwa ajili ya kuimarisha vikundi vya akina mama na watoto.