MKULIMA JEMBE WAPANIA KUFANYA MAKUBWA KWA KUTUMIA TEKNOLOJIA YA KISASA

Wanachama wa kikundi cha Mkulima Jembe wakitayarisha mashine ya umwagiliaji inayotumia mionzi ya jua, tayari kwa kuanza zoezi la kumwagilia bustani yao.

Na. Fedson Masawa

KIKUNDI cha Mkulima Jembe kilichopo kijiji cha Kastam, Kata ya Bukima ndani ya Jimbo la Musoma Vijijini, kimesema kwa sasa wana mpango mathubuti wa kuanzisha kilimo kwa ajili ya mazao ya chakula ili kupambana na hali mbaya ya upungufu wa chakula ndani ya jimbo hilo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi alipotembelea shamba la kikundi hicho, Mwenyekiti wa Mkulima Jembe Festo Obedi alisema, kikundi chao kilianza kwa kutumia teknolojia ya asili; yaani walitumia kubeba ndoo za maji kwa ajili ya kumwagilia bustani ndogo ndogo, lakini baadae walipokea mashine kutoka kwa Mbunge wao Prof. Sospeter Muhongo na kuanza kilimo cha kumwagilia kwa kutumia zana za kisasa.

“Kwa jitihada kubwa za kikundi, kwa sasa tumenunua mashine mbili ambazo zinatumia teknolojia ya umeme wa jua (Mashine zinazovuta na kusukuma maji kwa kutumia mionzi ya jua)” alisema Obedi.

Obedi alisema, kikundi chao kina mipango mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutumia mashine tatu walizonazo ili kufanya mambo makubwa na ya kushangaza, mambo hayo ni pamoja na kupanua mashamba kwa ajili ya kuanza kilimo kikubwa cha umwagiliaji ili kuzalisha mazao ya chakula kwa wingi ikiwa ni hatua njema ya kupambana na tatizo kubwa la upungufu wa chakula ndani ya jimbo la Musoma vijijini.

Kiongozi huyo alisema, wanafikiria kupata mashamba makubwa ya kukodi kwa ajili ya kufanikisha malengo waliyojiwekea. Pamoja na mipango hiyo muhimu Festo amesema changamoto kubwa ni mtaji wa kutekeleza na kufanikisha mipango yao ambapo ameomba serikali, wadau mbalimbali pamoja na Mbunge wao wa Jimbo la Musoma Mjini Prof. Sospeter Muhongo kuwasaidia kutatua changamoto hizo.

“Tuna mpango wa kukodi mashamba makubwa zaidi ili kufikia malengo tuliyoyaweka, lakini changamoto kubwa inayotusibu ni mtaji. Tunaomba kama serikali na wadau wengine kwa kupitia mbunge wetu watusaidie mtaji” aliomba Obedi.

Akizungumzia hali ya kujituma kwa vikundi vingine, Obedi alisema endapo vikundi vingine vilivyonufaika na mfuko wa jimbo na vile ambavyo havikunufaika na fedha hiyo kwa sasa, vikiwezeshwa kwa mashine hizo za kutumia mionzi ya jua, basi wanaamini jimbo la Musoma vijijini halitakuwa jimbo la kuomba na kuagiza chakula kutoka maeneo ya nje.

“Mashine hizi ni nzuri, tunaomba serikali kama itaamua kutuwezesha tena pamoja na vikundi vingine basi watununulie mashine kama hizi ili wanavikundi wengine waweze kushiriki kikamilifu” alisema.

Kwa upande wake Witness John amewaomba akinamama kuchangamkia fursa ya kilimo cha umwagiliaji kwani hakuna tena kilimo kitakachomkomboa mwanamke wa kijijini tofauti na kilimo cha umwagiliaji.

Witness aliongeza kuwa, hali ya hewa imekuwa ya kubadilika badilika, mwanzo walitegemea mvua za vuli na masika, lakini bado zimekuwa za kusuasua.

“Sisi wanawake, tunafanya kazi kwa bidii na inatusaidia kusomesha watoto, nawaombeni wanawake wenzangu tuchangamkie kilimo hiki cha umwagiliaji kwenye vikundi vingine ili tujikwamue katika umaskini tulionao na tuwasomeshe watoto wetu” alisema Witness.

Hata hivyo, Witness aligusia suala la viongozi wa kilimo kushindwa kuwafikia wana vikundi wakati wote wa kuanza kilimo hadi wakati wa mavuno, jambo ambalo alidai linachangia kushindwa kutatua changamoto za kitaalamu zinazowakabili wanapokumbana nazo ikiwa ni pamoja na ushauri wa kitaalamu, madawa yanayoweza kudhibiti magonjwa tofauti tofauti na namna ya kukabiliana nayo.