MUSOMA VIJIJINI WATAKIWA KUJITUMA NA KUFANYAKAZI KWA BIDII

Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Muhongo akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kiriba.

Na. Ramadhani Juma

MBUNGE wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter  Muhongo, amewataka wananchi wa jimbo hilo kujituma na kufanyakazi kwa bidii ili kukabiliana na njaa.

Prof. Muhongo alitoa kauli hiyo wakati wa sherehe za pasaka ambapo alipata fursa ya pekee ya kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Mwiringo, Bwai Kumusoma na shule ya msingi Kiriba.

Katika kusheherekea sikukuu hiyo, Prof. Muhongo pia alipata fursa muhimu ya kushiriki chakula cha pamoja na wananchi wa jimbo lake katika viwanja vya shule ya msingi Kiriba kijijini Kiriba na kuhudhuriwa na wananchi wengi.

Awali, akikagua ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Bwai Kumusoma, Prof. Muhongo alijiridhisha na ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na ofisi moja iliyojengwa kwa nguvu za wananchi ambapo katika ujenzi huo, Mbunge alichangia mabati 54 na mbao 149.

Baada ya kuguswa na jitihada za wananchi wa kijiji cha Bwai Kumusoma, Prof. Muhongo aliwaomba wananchi waliohudhuria katika ziara hiyo kujitokeza kwa moyo mmoja ili kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa shuleni hapo, ambapo wananchi hao walichangia kiasi cha 1,500,000/= na Prof. Muhongo alichangia mabati 200 kwa ajili ya kukamilisha zoezi la ujenzi wa vyumba vya madarasa shuleni hapo.

Akizungumzia suala la kuinua elimu jimboni, Prof. Muhongo ameitaka jamii ya Musoma vijijini isimame kidete kuhakikisha watoto wao wanapata elimu bora katika mazingira bora ili kuboresha ufaulu na kuongeza idadi ya wasomi wa elimu ya juu na hatimaye kuondokana na umaskini na njaa katika familia zao.

Pia Prof. Muhongo aliongeza kuwa, haina haja ya kuwa na shule nyingi zisizo bora, ni bora kuwe na shule chache zilizo na ubora kitaaluma na kimazingira ya kujifunzia na kufundishia.

“Tukisomesha watoto wetu tutaondokana na umaskini na familia iliyo na msomi hawana njaa. Pia tusiwe na utitiri wa shule zisizo na ubora” alisema Prof. Muhongo.

Aidha, Prof. Muhongo aliwahimiza wananchi wa Musoma vijijini kujituma katika shughuli za kilimo cha umwagiliaji ili kuondokana na tatizo la njaa katika maeneo yao.

Prof. Muhongo alisema, inasikitisha kuona mikoa mingine inapata chakula cha kutosha wakati Musoma walio katika eneo la kandokando mwa ziwa wanakosa chakula.

“Ni jinsi gani tunavyochekwa na watu wa mikoa mingine kuona tunalia njaa wakati tuna ziwa. Tujitume kufanya kazi, serikali haiwezi kulisha watu milioni 50” alisema Prof. Muhongo.