MBUNGE MUSOMA VIJIJINI AFANYA ZIARA YA KUKAGUA UJENZI WA MADARASA

Mtendaji wa kijiji cha Bugoji Yuda Magoma (kulia) akitoa taarifa ya maendeleo ya shughuli za ujenzi katika shule ya msingi Kanderema. Kushoto, aliyevaa fulana ya kijani ni Prof. Muhongo.

Na Mwandishi Wetu

MBUNGE wa jimbo la Musoma vijijini na Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo, amekagua ujenzi wa vyumba vya madarasa unaoendelea kwa kasi kubwa ndani ya jimbo lake.

Katika ziara yake hiyo, Prof. Muhongo aliongozana na  viongozi mbalimbali wa serikali na vyama, ambapo walipokelewa kwa nyimbo kutoka kwa Miriam Mwangwa (8), akihamasisha wazazi kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa vyumba vya madarasa, kuachana na majungu ya vijiweni pamoja na kuwaasa wanafunzi kujituma katika masomo yao.

Tukio hilo liliwashangaza wananchi wengi na viongozi waliohudhuria katika viwanja hivyo na kuhamasika kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo huku Prof. Muhongo akielezea kuvutiwa na ujumbe wa binti huyo na kuahidi kuungana na wananchi wa Bugoji ili kutatua changamoto ya vyumba vya madarasa.

Akiwasili katika kata ya Bugoji, Prof. Muhongo alikagua ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa, ofisi mbili za walimu na jengo la maktaba katika shule ya msingi Kanderema ambapo ujenzi huo umefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa msaada wa mbunge aliyetoa mifuko 120 ya saruji huku wananchi wakijitolea kufanya kazi mbalimbali za kusaidia ujenzi huo.

Akizungumzia shughuli za ujenzi wa vyumba vya madarasa, diwani wa kata ya Bugoji Ibrahimund Malima, alimshukuru mbunge wao kwa msaada aliowapatia hususani saruji na mabati.

Vilevile diwani alimshukuru kwa kuwasaidia mbegu za alizeti na mihogo, na kuahidi kusimamia kikamilifu na kuhakikisha vifaa vyote vilivyotolewa na mbunge na wahisani wengine vinafanya kazi iliyopangwa.

Akiwa katika kijiji cha Muhoji, Prof. Muhongo alikagua ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa katika shule ya msingi Muhoji vilivyojengwa kwa nguvu za wananchi wa kijiji hicho ambapo wananchi walichangia ununuzi wa saruji na mbao.

“Vyumba vyote vinne vimejengwa kwa nguvu za wananchi pia mbao zote ni nguvu za wananchi, hivyo tunaomba mbunge kama kuna uwezekano tunaomba utusaidie bati 108 tukamilishe ujenzi huu kama ulivyotusaidia bati za kuezeka chumba kimoja kilichokamilika” alisema mtendaji wa kijiji cha Muhoji, Mohamed Hamza.

Aidha, mtendaji huyo aliongeza kuwa, kijiji cha Muhoji kina changamoto ya ukosefu wa zahanati jambo ambalo lilimgusa pia Prof. Muhongo na kuamua kuungana na wananchi wa kijiji hicho kuanzisha harambee kwa ajili ya ujenzi wa zahanati.

Katika harambee hiyo, jumla ya 480,000/= zilipatikana. Prof. Muhongo pia aliwaunga mkono kwa kuwasaidia jumla ya mifuko 100 ya saruji na kuwataka wafuate taratibu zote za kitaalamu katika ujenzi wa zahanati hiyo.

Mbali na zoezi hilo la ukaguzi wa ujenzi wa madarasa, Prof. Muhongo alihudhuria zoezi la kuaga mwili wa mwalimu mkuu wa shule ya msingi Chumwi Edward Kohe, lililofanyika shuleni hapo.

Katika kumuenzi mwalimu huyo, Prof. Muhongo aliahidi wananchi wa kijiji cha Chumwi kuwajengea vyumba 9 vya madarasa kwa kuwapatia mifuko 405 ya saruji. Prof. aliwataka wananchi kujituma kwa kujenga vyumba hivyo kama ishara ya kumkumbuka mwalimu huyo daima.

“Mwalimu amefariki lakini historia yake haitopotea milele. Tukijenga hivyo vyumba vya madarasa, mwalimu hatosahaulika milele” alisema Prof. Muhongo.