MBEGU ZA MKOMBOZI ZALETA MATUMAINI KWA WAKULIMA MUSOMA VIJIJINI

Afisa kilimo kutoka idara ya kilimo halmashauri ya wilaya ya Musoma (kushoto) akikagua moja ya mashina yaliyo ng’olewa katika shamba la mbegu bora aina ya mkombozi katika shamba la shule ya msingi Butata kijijini Butata. Kulia ni Charles Buremo afisa mtendaji wa kijiji hicho na katikati ni Mshangi Salige, afisa kilimo kata ya Bukima na Rusoli.

Na Mwandishi Wetu

MBEGU bora za mihogo aina ya Mkombozi ambazo zilisambazwa mwishoni mwa mwaka jana, zimeonekana kustawi na kuleta matumaini kwa wakulima wa Musoma vijijini.

Hayo yamebainika wakati wa zoezi la usambazaji wa mbegu za awamu ya pili ambazo zimetolewa na Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo, zoezi ambalo limefanywa na Afisa kilimo kutoka halmashauri ya wilaya ya Musoma na Msaidizi wa Mbunge Fedson Masawa.

Baada ya zoezi hilo kukamilika, viongozi hao waliomba kutembelea baadhi ya mashamba darasa yaliyopo shule ya msingi Kwikerege pamoja na shule ya msingi Butata na kujiridhisha na maendeleo ya mbegu hizo zilizotolewa na Halmashauri kwa mara ya kwanza.

Akitoa taarifa ya ustawi wa mbegu hizo, mwalimu Maregesi Malima ambaye ni mwalimu wa bustani katika shule ya msingi Kwikerege alisema, mbegu aina ya mkombozi zinastawi vizuri ila changamoto kubwa iliyowakabili ni ukosefu wa mvua kwa kipindi kirefu.

Mwalimu Malima alisema, hali hiyo imechangia mbegu kukauka, ingawa wana imani ya kupata mavuno mazuri hasa kwa awamu ya pili.

Akizungumzia kuhusu namna ya utunzaji na usimamizi wa mashamba hayo, Afisa kilimo wa kata ya Rusoli na Bukima Mshangi Salige alisema, wanafuatilia kwa ukaribu na kusimamia kuanzia hatua ya uandaaji wa mashamba, mbegu na upandaji.

Salige aliongezea kuwa, kwakuwa wafanyakazi wakuu wa mashamba hayo ni wanafunzi, wanatumia muda mwingi pia kuwa karibu nao hasa wawapo shambani wakati wa kupanda na kupalilia.

“Mimi kama msimamizi wa kilimo kwenye kata hizi mbili wajibu wangu ni kusimamia hatua zote kuanzia kuandaa shamba hadi kupalilia. Pia kuwasimamia vizuri wanafunzi katika hatua ya upandaji na upaliliaji ili wasiende kinyume na kanuni za kilimo” alisema Salige.

Naye afisa kilimo kutoka wilaya ya Musoma Godfrey Katima, alielezea kukerwa na kitendo cha baadhi ya wananchi wa kijiji cha Butata kung’oa mihogo hiyo mashambani bila utaratibu wowote hali ya kuwa haijafikia hatua ya kuvunwa na kusema hivyo ni vitendo visivyovumilika.

“Viongozi msiwavumilie hata kidogo wale wote watakaobainika kung’oa mihogo hiyo na hatua kali zichukuliwe dhidi yao na kila raia awe mlinzi wa mbegu hizi ili zitusaidie wengi hapo baadae” alisema Katima.

Akizungumza wakati wa kukamilisha zoezi la ukaguzi wa mashamba hayo, Mtendaji wa kijiji cha Butata Charles Buremo kwa niaba ya wananchi wa kijiji cha Butata na jimbo la Musoma vijijini, amemshukuru Prof. Muhongo kwa kuwathamini wananchi wake na kuwaletea mbegu bora zaidi za mihogo ili kuondokana na upotevu wa zao hilo jimboni.

Pia Buremo amekiri kuwepo kwa vitendo vinavyofanywa na baadhi ya watu katika mashamba hayo ya mbegu bora na kuahidi kuyashughulikia matendo hayo ili kuhakikisha yanakoma hapo kijijini kwake.

“Kwanza nimshukuru Prof. Muhongo kwa namna anavyowajali wananchi wake na kuwaletea mbegu hizi bora za mihogo ili kuendelea kulinda heshima ya zao hili jimboni. Ni kweli, matendo haya yatakuwa yanafanywa na watu wasio na maono na nia njema ya kuthamini umuhimu wa mbegu hizi. Mimi nina ahidi kulishughulikia suala hili kwa ajili ya manufaa ya wengi hapo baadaye” alisema Buremo.