MBUNGE WA MUSOMA VIJIJINI AKAGUA MAENDELEO YA UJENZI WA MADARASA

 

Mbunge wa Musoma vijijini na Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo (mwenye fulana nyeusi) akishirikiana na wananchi wa kijiji cha Kome kwenye ujenzi unaoendelea wa vyumba 10 vya Madarasa. Mbali na kushiriki ujenzi huo, Prof. Muhongo alitoa msaada wa mifuko na bati kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyumba hivyo.

Mbunge wa Musoma vijijini na Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo (mwenye fulana nyeusi) akishirikiana na wananchi wa kijiji cha Kome kwenye ujenzi unaoendelea wa vyumba 10 vya Madarasa. Mbali na kushiriki ujenzi huo, Prof. Muhongo alitoa msaada wa mifuko na bati kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyumba hivyo.

Na Fedson Masawa

MBUNGE wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Muhongo amekagua maendeleo ya ujenzi katika shule ya msingi Kome “B” iliyopo kijiji cha Kome kata ya Bwasi.

Akizungumza shuleni hapo, Prof. Muhongo alisema ameridhishwa na hatua nzuri iliyofikiwa na wananchi wa kijiji cha Kome, kwa kuweza kujenga jumla ya vyumba sita vya madarasa hadi usawa wa lenta huku malengo yakiwa ni kujenga vyumba 10.

“Tukitaka kufanikiwa lazima twende kwa mpango. Hatuwezi kuwa na maendeleo wakati tunakuwa na mipango ya kwenda na kurudi, kwenda na kurudi nyuma” alisisitiza Prof. Muhongo.

Aidha Prof. Muhongo amewathibitishia wananchi kuwa, mifuko mingine ya saruji itawasili Musoma baada ya wiki mbili na kuwasisitiza viongozi na wananchi kujituma kuhakikisha saruji hiyo ikifika inatumika haraka iwezekanavyo, tofauti na hivyo mifuko itahamishwa na kupelekwa kwingine.

“Baada ya wiki mbili nitatoa mifuko mingine ya saruji na mkipewa saruji au mabati, msipovifanyia kazi vitahamishwa” alisisitiza Prof. Muhongo.

Akizungumzia suala la umeme na kilimo cha umwagiliaji kama lilivyo wasilishwa na wananchi wa kijiji cha Kome, Prof. Muhongo amewaondoa wasiwasi na kusema watapata umeme wa kutosha kwa kuwa bado hatua ya kusambaza umeme vijijini inaendelea.

“Ndugu zangu kuhusu umeme msiwe na wasiwasi, umeme unakuja wa kutosha na suala la umeme tunaenda awamu kwa awamu, ndani ya miaka mitano vijiji vyote vya Tanzania vitakuwa vimenufaika na umeme” alisema Prof. Muhongo.

Kuhusu suala la kilimo, Prof. Muhongo amekiri kuwepo na ukame jimboni na maeneo mengine na kuona umuhimu wa kutumia kilimo cha umwagiliaji kwa jamii zote zinazoishi kando kando mwa ziwa ambapo amemuagiza Mwenyekiti wa halmashauri na madiwani wote kulijadili na kuona namna ya kuzisaidia jamii hizo ili kuondokana na tatizo la njaa kuliko kutegemea msimu wa mvua pekee.

Naye mwenyekiti wa Halmashauri ya Musoma Charles Magoma, amemthibitishia Prof. Muhongo kuwa suala la ujenzi wa vyumba vya madarasa wataendelea kulisimamia na kufuatilia matumizi sahihi ya vifaa hivyo na kuhakikisha vinatumika kwa wakati.

Magoma ameahidi kuwasilisha hoja ya ununuzi wa mashine kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji kwa jamii zinazoishi kandokando mwa ziwa Viktoria ili waweze kujinusuru na tatizo la njaa.

“Ndugu mheshimiwa, mimi naamini yote uliyoyazungumza tutayafanyia kazi, vifaa vya ujenzi tutaendelea kuvifuatilia na suala la mashine tutalijadili kwenye vikao vyetu vya mipango na fedha ndani ya siku mbili zijazo” alisema Magoma.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Bwasi, Masatu Nyaonge, amemshukuru Prof. Muhongo kwa kuweza kufika kijijini hapo ili kujionea kazi nzuri inayofanywa na wananchi wake na kumhakikishia kuwa pamoja na wananchi wake kukumbwa na tatizo la njaa, lakini bado hawajakata tamaa ya kufanya maendeleo na bado wana uhitaji wa vifaa vya ujenzi kijijini hapo.