MASHINDANO YA MITUMBWI MUSOMA VIJIJINI YAMALIZIKA

sita

Vijana kutoka Kata ya Suguti ambao walishika nafasi ya Tatu wakishangilia mara baada ya mtumbwi wao kuwasili kwenye eneo la kumalizia mashindano.

Na. Hamisa Gamba

MASHINDANO ya mitumbwi Musoma vijijini yaliyoshirikisha timu 12 yamemalizika kwa Kata ya Etaro kuibuka na ushindi na hivyo kujinyakulia fedha tasilimu milioni moja pamoja na kombe.

Mashindano hayo yaliandaliwa na Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo kwa ajili ya kuuaga mwaka 2016 na kuukaribisha mwaka 2017 ambapo washindi wa pili ambao ni Kata ya Nyakatende walijinyakulia shilingi 750,000 na washindi wa tatu ambao ni Kata ya Suguti kujinyakulia shilingi 500,000 na huku wanaofuatia walipata shilingi 20,000 kwa kila Kata.

Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Musoma Vijijini na Diwani wa Kata ya Mugango, Charles Magoma, alimpongeza Profesa Muhongo kwa kuanzisha mashindano ya namna hiyo jimboni humo kwani yamekutanisha wananchi wa Musoma Vijijini kutoka pande mbalimbali za jimbo hilo.

Aliongeza kwamba mashindano hayo yameleta mwamko mkubwa miongoni mwa vijana hasa ikizingatiwa kuwa hakuna mashindano ambayo huwakutanisha vijana kwa wingi kama ilivyokuwa kwa mashindano hayo ya mtumbwi.

Kwa upande wake, mbunge wa jimbo hilo, Profesa Sospeter Muhongo alisema aliamua kuandaa mashindano hayo na mengine ya ngoma za asili na kuimba kwaya ili kuwakutanisha wanamusoma vijijini kwa maendeleo ya afya zao na jimbo kwa ujumla.

Alisema njia mojawapo ya kuwa na afya bora ni kushiriki michezo mbalimbali na hivyo aliahidi mashindano mengine ya mieleka ambayo yatafanyika kwenye Kata ya Mugango mapema mwezi Aprili.

Aliwataka wananchi hususani vijana kujitokeza kwa wingi na kwamba washindi watapewa zawadi ambayo alisema ataitangaza siku nyingine.

Aidha, alisema kila Kata iandae washiriki wawili kwa ajili ya kushiriki mieleka na wananchi wajiandae kushuhudia mashindano hayo ya kihistoria kuwahi kutokea Musoma Vijijini.

Mashindano hayo ya mitumbwi jimboni humo yalishirikisha jumla ya Kata tisa huku kila mtumbwi ukiwa na washiriki kati ya watano hadi saba na vilevile timu moja ya kimataifa ya rafiki zake na mbunge huyo kutoka Ujerumani ilishiriki na kushika nafasi ya mwisho.