‘MSIWE NA WASIWASI, HAKUNA MTU ATAKAYEKUFA KWA NJAA’

unnamed

Wananchi wa Kata ya Nyakatende wakichukua chakula kilichoandaliwa kwa ajili ya sherehe ya Krismasi.

Na. Fedson Masawa

MBUNGE wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo amewahakikishia wananchi wake kwamba, hakuna atakayekufa kwa njaa licha ya ukame wa muda mrefu unaowakabili.

Prof. Muhongo alisema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Nyakatende muda mfupi kabla ya chakula cha mchana cha pamoja na wananchi wa jimbo lake katika kusheherekea sikukuu ya krismasi.

Alisema, serikali imeshalitambua tatizo la njaa linalowakabili wananchi wa jimbo hilo na itawaletea chakula cha bei nafuu, hivyo hakuna hata mtu mmoja atakayekufa njaa.

“Kwa hiyo ndugu zangu, serikali inalitambua tatizo lenu, msiwe na wasiwasi, hakuna mtu atakayekufa kwa njaa, serikali itatatua tatizo hilo” alithibitisha Prof. Muhongo.

Aidha, akizungumzia kilimo cha alizeti, kilimo cha umwagiliaji pamoja na mbegu za mihogo, Prof. Muhongo amesisitiza kuwa, kwa mkulima yeyote anayehitaji mbegu za alizeti atoe taarifa ili kuongezea mbegu hizo.

Mbali na hilo, alisema fedha za mfuko wa jimbo zitaelekezwa kwenye vikundi vya umwagiliaji pamoja na kununua mbegu za mihogo ili kupambana na tatizo la njaa.

“Zile fedha za mfuko wa mbunge ambazo tumepata zaidi ya milioni 38, zote tutajadili kuziweka kwenye kilimo ili tutatue matatizo ya njaa kwenye jimbo lenu” alisema Prof. Muhongo.