SERIKALI YATOA MCHANGO MKUBWA WA TSH MILIONI 573 KWENYE UJENZI WA WANYERE SEKONDARI

Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo akiwa na Wanakijiji kwenye Mkutano uliofanyika jana Kijijini hapo kwenye eneo la ujenzi wa Sekondari mpya, ambayo inajengwa ndani ya Kitongoji cha Mwikoro, Kijijini Wanyere, Kata ya Suguti, Musoma Vijijini.

Jimbo la Musoma Vijijini laendelea kutatua matatizo yanayowakabili wanafunzi wanaosoma kwenye Sekondari za Kata za Jimboni humo.

Matatizo makuu yanayowakabili ni:
*umbali mrefu wa kutembea kwenda masomoni
*mirundikano ya wanafunzi madarasani
*upungufu au ukosefu wa maabara za masomo ya sayansi
*ukosefu wa maktaba
*upungufu mkubwa wa walimu, hasa wa masomo ya Sayansi na Lugha.

Ujenzi wa Sekondari mpya Kijijini Wanyere:
Kijiji cha Wanyere ni moja ya vijiji vinne (Chirorwe, Kusenyi, Suguti na Wanyere) vya Kata ya Suguti yenye Sekondari moja iliyoko Kijijini Suguti

Wanafunzi wa Kijiji cha Wanyere wanalazimika kutembea zaidi ya KILOMITA 30 kwenda na kurudi kutoka masomoni kwenye Sekondari yao ya Kata. Baadhi ya wanafunzi wamepanga vyumba (na wanajipikia) karibu na eneo la shule hiyo.

Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo alitembelea Kijiji cha Wanyere kwa malengo makuu mawili:

*kupokea kero za Wanakijiji na kuzitatua
*kuhamasisha ujenzi wa sekondari mpya kijijini hapo.

Michango ya ujenzi wa Wanyere Sekondari:
Mbunge Prof Muhongo aliendesha HARAMBEE ya kuanza ujenzi huo na michango iliyotolewa ni kama ifuatavyo:

Wanakijiji wa Wanyere wameanza kuchangia:
*Nguvukazi za kusomba mchanga, mawe, maji na kuchimba msingi wa jengo moja la Madarasa 2 na Ofisi 1 ya Walimu

*Fedha taslimu takribani Tsh milioni 2.5

Wanakijiji wa Kataryo:
*Saruji Mifuko 30 imetolewa na Kijiji jirani cha Kataryo cha Kata jirani ya Tegeruka. Watoto wa Kijiji hiki jirani wanasoma Kijijini Wanyere.

Mbunge wa Jimbo:
*Saruji Mifuko 100 - Prof Muhongo ameanza kutoa michango yake kwa kuchangia saruji hiyo.

Halmashauri yetu (Musoma DC):
*bado haijatoa mchango wo wote!

Serikali Kuu (TAMISEMI):
Bajeti ya Mwaka 2023/2024, Serikali itatoa Tsh Milioni 573 kupitia Mradi wake wa SEQUIP kwa ajili ya ujenzi wa Sekondari mpya Kijijini Wanyere. Hii itakuwa Sekondari ya pili ya Kata ya Suguti.

Wananchi na Viongozi wa Jimbo la Musoma Vijijini wanaishukuru Serikali, chini ya uongozi mzuri wa Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuongeza ubora wa utoaji wa elimu Jimboni mwao.

Usisahau kutembelea TOVUTI ya Jimbo letu ambayo ni:
www.musomavijijini.or.tz

Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Musoma Vijijini
www.musomavijijini.or.tz

Tarehe:
Alhamisi, 1.6.2023