SEHEMU YA PILI YA TAARIFA YA KIKAO CHA MBUNGE WA JIMBO NA WAKUU WA SHULE ZA MUSOMA VIJIJINI

 Walimu Wakuu wa Sekondari za Musoma Vijijini wakiwa na Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini kwenye Kikao chao cha tarehe 3.2.2023 kilichofanyika Busambara Sekondari, Kijijini Kwikuba.

Sehemu ya Kwanza ya Taarifa ya Kikao hicho:

Sehemu hii ilitolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo.

*Mahali inapopatikana ni kwenye TOVUTI ya Jimbo letu ambayo ni:
www.musomavijijini.or.tz

SEHEMU YA PILI - UFAULU WA FORM II & IV (2020, 2021& 2022)

*Kwa nini ufaulu siyo mzuri kwenye Sekondari zetu za Musoma Vijijini?

*Nini kifanyike kuongeza UELEWA na UFAULU kwa wanaojifunza (WANAFUNZI)

*Nini kifanyike kuongeza UMAHIRI na UWAJIBIKAJI wa kufundisha kwa WALIMU wetu?

*Majukumu ya WAZAZI ni yapi?

(1) Matokeo yakutoridhisha ya Mwaka jana (2022)
*Kubadilika kwa mfumo wa utungaji wa mitihani unaozingatia umahiri, yaani, "competence based" badala ya ule mfumo uliozoeleka wa kukariri. Matayarisho ya mabadiliko hayo hayakuwepo.

(2) Matokeo ya kutoridhisha ya Miaka 3 mfululizo (2020, 2021 & 2022)

(2a) WANAFUNZI
*Kutembea umbali mrefu kwenda masomoni. Wapo wanaotembea zaidi ya kilomita tano (5) kwenda masomoni

*Wanafunzi kukosa chakula wawapo masomoni (kifungua kinywa & chakula cha mchana)

*Wapo wanafunzi waliopanga vyumba kwenye vijiji vya karibu na Sekondari wanazosoma. Hawa wanafunzi wapangaji wanaishi kwa kujitegemea kama ziishivyo kaya zetu.

*Sekondari nyingi hazina Maabara na Vifaa vyake kwa masomo ya sayansi (chemistry, physics & biology laboratories)

*Sekondari karibu zote hazina Maktaba. Vitabu vya Maktaba vipo vilivyotolewa na Mbunge wa Jimbo

*Uhaba wa vitabu vya kiada ambapo uwiano unapaswa kuwa kitabu kimoja (1) kwa mwanafunzi mmoja (1). Uwiano huo kwa sasa, kwa baadhi ya Sekondari, ni kitabu kimoja (1) kwa wanafunzi watano (5).

*Lugha ya kufundishia ya Kiingereza bado ni tatizo.

Hata lugha yetu ya Taifa (Kiswahili) bado uelewa na ufaulu wake hauridhishi.

(2b) WALIMU
*Upungufu mkubwa wa walimu ambao hauendani na uwiano wa walimu na wanafunzi (ratio: teacher/students). Kwa mfano ipo Sekondari ina wanafunzi 1,012 na walimu 13 tu! Ipo Sekondari mpya yenye wanafunzi 158 na walimu 5!

*Uhaba mkubwa wa walimu wa masomo ya sayansi. Kwa mfano, kuna Sekondari zenye mwalimu mmoja (1) tu wa Hisabati na mmoja (1) tu wa Fizikia kwa madarasa yote (Form I hadi IV)!

*Upungufu na uhaba mkubwa wa walimu unalazimisha Sekondari kufanya yafuatayo:
(i) kuajiri walimu wa kujitolea ambao wanalipwa posho na wazazi, na Mbunge wa Jimbo huwa anachangia kwa baadhi ya Sekondari
(ii) kuweka wanafunzi kati ya 50 na 60, au zaidi ndani ya chumba kimoja cha darasa ili kupunguza mizigo ya vipindi vyingi kwa baadhi ya walimu.

MAPENDEKEZO YA KUONGEZA UBORA WA KUJIFUNZA NA KUFUNDISHA KWENYE SHULE ZETU

(1) WANAFUNZI & WALIMU
*Mapungufu na mahitaji yaliyoelezwa hapo juu, kwa upande wa Wanafunzi & Walimu, yatatuliwe kwa ushirikiano wa Wahusika wote.

(2) WAZAZI
*Wazazi watimize wajibu wao wa malezi mazuri ya watoto wao, na wafuatilie kwa karibu sana mienendo na tabia za watoto wao, k.m. kushinda kwenye runinga (TV), kubeti, kamari na kucheza pool.

*Wazazi watimize wajibu wao wa kuwanunulia watoto wao mahitaji ya shule na elimu kwa ujumla.

*Wazazi wakubali kuchangia chakula cha mchana cha watoto wao wawapo masomoni.

*Wazazi waache kuwapa watoto wao kazi za kiuchumi za familia wawapo masomoni, kwa mfano, kuwatuma kuchunga mifugo, kuvua samaki, kuchimba madini, na kuuza bidhaa sokoni wakati wa vipindi masomoni.

*Sera ya ELIMU BILA MALIPO iendelee kufanunuliwa na Wahusika ili Wazazi wasiache kutimiza wajibu wao wa kuchangia upatikanaji wa elimu nzuri kwa watoto wao.

*Wazazi na Walimu waendelee kuboresha uhusiano kati yao kwa manufaa ya uboreshaji wa elimu itolewayo kwenye shule zao.

(3) WALIMU
*Walimu waongezewe mafunzo wawapo kazini. Mafunzo yatolewe mara kwa mara ndani ya kipindi kifupi cha miaka 2-3.

*Kuwepo msawazo sawa kwa wingi (fair distribution) wa walimu kwenye Sekondari za vijijini na mijini ndani ya Halmashauri, Wilaya na Mkoa.

*Maslahi ya walimu yaboreshwe kwa kiwango kikubwa, yaani:
(i) Walimu wajengewe nyumba za kuishi hasa wale wanaofundisha vijijini
(ii) Mishahara ya Walimu iboreshwe sana na makato yake yapunguzwe.

Nchi ambazo zinaongoza Dunia kwa ubora wa elimu, mishahara ya walimu wao iko juu kuzidi taaluma nyingi nchini humo!

*Kitengo cha uthibiti ubora kiongezewe uwezo wa kufuatilia shughuli za ufundishaji na ujifunzaji mashuleni

*Kuimarisha lugha za kufundishia na kujifunzia kwa shule za Msingi na Sekondari

*Kutoa motisha kwa wanafunzi na walimu wanaofanya vizuri kwenye mitihani inayotolewa.

*Waliopewa majukumu ya kiuongozi ya kusimamia masuala ya elimu kwenye mashule wawe na uwezo wa kielimu wa kutekeleza majukumu yao.

ELIMU NI UCHUMI
ELIMU NI MAENDELEO

Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Musoma Vijijini
www.musomavijijini.or.tz

Tarehe:
Jumatatu, 20.2.2023