KATA YA KIRIBA YAANZA UJENZI WA SEKONDARI YA PILI

Picha zilizoko hapa zinaonesha baadhi ya Wananchi wa Kijiji cha Bwai Kumsoma wakiwa kwenye ujenzi wa Sekondari yao mpya, BWAI SEKONDARI, inayotarajiwa kufunguliwa mwakani (Januari 2022). Hii itakuwa SEKONDARI ya PILI ya Kata ya Kiriba.

Tarehe 21.5.2021
Jimbo la Musoma Vijijini
Na: Hamisa Gamba
Msaidizi wa Mbunge
UMBALI MREFU wa kutembea na MIRUNDIKANO ya Wanafunzi madarasani ni sababu kuu zinazofanya baadhi ya KATA za Jimbo la Musoma Vijijini KUAMUA kuwa SEKONDARI zaidi ya moja.
KATA ya KIRIBA inayoundwa na Vijiji vitatu (3) ambavyo ni Bwai Kwitururu, Bwai Kumsoma, na Kiriba ina Sekondari moja ya Kata (KIRIBA SEKONDARI) iliyojengwa Kijijini Bwai Kwitururu.
SEKONDARI hii ilifunguliwa Mwaka 2006, na ina jumla ya WANAFUNZI 731 (Kidato cha 1-4).
WANAFUNZI wa Vijiji vya Bwai Kumsoma na Kiriba wanalazimika kutembea umbali wa kati ya KILOMITA 5 hadi 12 kwenda masomoni KIRIBA SEKONDARI.
Vilevile, kuna MIRUNDIKANO mikubwa ya Wanafunzi madarasani. Kwa mfano, Wanafunzi wa KIDATO cha KWANZA wako sitini (60) ndani ya chumba kimoja cha darasa
WANANCHI WAAMUA KUJENGA SEKONDARI YA PILI YA KATA
KIJIJI cha  Bwai Kumsoma chenye WAKAZI 10,500 KIMEAMUA kujenga SEKONDARI yake ili KUTATUA MATATIZO yaliyotajwa hapo juu.
SEKONDARI inayojegwa na KIJIJI kimoja hiki, chenye VITONGOJI NANE (8), itaitwa BWAI SEKONDARI na inajengwa ndani ya KITONGOJI cha BUSIKWA
WANAFUNZI wa kujiunga na SEKONDARI inayojengwa wapo wa kutosha kwani Kijiji cha Bwai Kumsoma kina SHULE za MSINGI TATU (3), na Wanafunzi wa Vijiji vingine viwili vya Kata hii watakaribishwa kujiunga na BWAI SEKONDARI inayotarajiwa kufunguliwa mwakani (Januari 2022).
MAOTEO ya WANAFUNZI watakaojiunga na  Kidato cha Kwanza mwakani (Januari 2022) kwenye Sekondari hii mpya ni kati ya 150 na 170.
MABOMA YANAYOJENGWA KWENYE SEKONDARI MPYA
Mwenyekiti wa Serikali ya  Kijiji cha Bwai Kumsoma, Ndugu PIMA MASINDE KITUNDU  ameeleza kwamba
ujenzi wa Shule hii ulianza rasmi mwezi uliopita (Aprili 2021), na unatekelezwa kwa mpangilio ufuatayo:
*Boma la Vyumba 3 vya Madarasa
*Vyoo vya Wanafunzi na Walimu
*Boma la Jengo la Utawala
*Maabara 3 (Fizikia, Kemia na Bailojia)
*Boma la Nyumba ya Mkuu wa Shule
MTENDAJI KATA, Ndugu  Pendo Isaach Mwita, na MRATIBU ELIMU KATA, Mwl Beatrice Ndosi, wanafuatilia kwa karibu sana ujenzi wa Sekondari hii mpya  – TUNAWASHUKURU SANA!
WACHANGIAJI WA MRADI HUU WA UJENZI.
MICHANGO itatolewa kwa awamu mbalimbali na kwa kuanzia:
*NGUVUKAZI za Wanakijiji zitatumika kusomba mawe, kokoto, mchanga na maji.
*FEDHA taslimu, Tsh 10,000/= kwa kila mkazi mwenye umri kati ya miaka 18 na 59
*DIWANI wa Viti Maalum, Ndugu FLORA MAGWA ameanza kuchangia kwa kutoa SARUJI MIFUKO 5 (mitano)
*MBUNGE wa Jimbo, Prof Sospeter Muhongo ameanza kuchangia kwa kutoa SARUJI MIFUKO 50 (hamsini)
ELIMU NI KIPAUMBELE CHA KWANZA MUSOMA VIJIJINI (KATA 21)
*Tunazo Sekondari 21 za Kata
*Tunazo Sekondari 2 za Binafsi
*Tunajenga Sekondari Mpya 8
WANAKIJIJI WANAOMBA TUSHIRIKIANE NAO KUJENGA SEKONDARI MPYA
MWENYEKITI Ndugu Pima Masinde Kitundu kwa niaba ya Wananchi na Serikali ya Kijiji cha Bwai Kumsoma anaomba WADAU wa MAENDELEO wakiwemo WAZALIWA wa KATA ya KIRIBA wajitokeze kuchangia MRADI huu wa ujenzi wa SEKONDARI ya pili ya Kata yao.
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Musoma Vijijini