KIJIJI CHA ETARO CHAJIWEKA SAWA KUMALIZA TATIZO LA UPUNGUFU WA VYUMBA VYA MADARASA

Mwalimu Mkuu wa S/M Etaro (Mwl Mangire Stephano Mahombwe) na Mtendaji wa Serikali ya Kijiji cha Etaro (Ndugu Sophia Charles) wakiwa kwenye eneo la ujenzi wa Vyumba vipya vya Madarasa.

Na: Fedson Masawa
Msaidizi wa Mbunge
WANANCHI wa Kijiji cha ETARO, Kata ya Etaro wanaendelea na utekelezaji wa AZIMIO la MKOA WA MARA LA UBORESHAJI WA MIUNDOMBINU YA ELIMU katika Shule yao ya Msingi (S/M Etaro).
UTARATIBU MAALUMU unawekwa wa kuwashirikisha WADAU mbalimbali wa Maendeleo wakiwemo WAZALIWA wa Kijiji  na Kata hiyo ili waweze KUCHANGIA utatuzi wa tatizo SUGU  la UPUNGUFU wa Miundombinu ya Elimu Shuleni hapo.
Akizungumza na Msaidizi wa Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Shuleni hapo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Etaro, Mwl Mangire Stephano Mahombwe alisema kuwa S/M Etaro ilianzishwa Mwaka 1995, ina jumla ya WANAFUNZI 1,014. Mahitaji ni Vyumba 26 vya Madarasa, vilivyopo ni 10, upungufu ni Vyumba 16 vya Madarasa.
Mwalimu Mahombwe ameongezea kuwa,  Vyumba vipya Vinne (4) vinavyojengwa vikikamilika, Shule hiyo itakuwa BADO na UPUNGUFU wa Vyumba 12 vya Madarasa.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Etaro, Ndugu Sophia Charles alisema Serikali ya Kijiji cha Etaro inaendelea KUHAMASISHA WANANCHI wa Kijiji hicho na WADAU wa Maendeleo wakiwemo WAZALIWA wa Kijiji na Kata hiyo kuendelea KUCHANGIA UJENZI huo. HARAMBEE ya Mbunge wa Jimbo, Prof Sospeter Muhongo itapigwa hivi karibuni.
Mtendaji wa Kijiji hicho alitaja VIFAA vya UJENZI vinavyohitajika kwa ujenzi unaondelea kwa wakati huu kuwa ni Mabati 54, Saruji Mifuko 280, Milango na Madirisha.
MICHANGO YA AWALI YA MBUNGE WA JIMBO
Kwenye Shule hiyo Mbunge wa Jimbo, Prof Sospeter Muhongo ALISHACHANGIA:
* Madawati 227
* Vitabu vingi vya Maktaba
* Saruji Mifuko 60
MICHANGO KUTOKA MFUKO WA JIMBO
* Mabati 244 ambayo yameezeka Vyumba 4 vya Madarasa na Ofisi moja (1) ya Walimu
Diwani wa Kata ya Etaro, Mhe Paul Charamba ameishukuru sana SERIKALI kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kwa usimamizi na ufuatiliaji mzuri wa Miradi ya Maendeleo ndani ya Kata ya Etaro.
Aidha, Diwani huyo amemshukuru sana Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo kwa MICHANGO yake na namna anavyowashirikisha Wananchi Jimboni humo katika kufanikisha utekelezaji wa Miradi yao ya Maendeleo, ikiwemo ya Kata ya Etaro.
KARIBUNI TUCHANGIE MIRADI YA ELIMU KIJIJINI ETARO