MVUA YASABABISHA MAAFA MENGINE KIJIJI CHA BUKUMI NA BURAGA

Walimu na uongozi wa Shule ya Msingi Bukumi na wananchi wa kijiji hicho wakikagua athari zilizotokana na mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali na kusababisha paa za vyumba vya madarasa vya shule hiyo kuezuliwa huku familia tisa zikikosa makazi kwenye kijiji cha Bukumi na Buraga.

Na. Fedson Masawa

MVUA kubwa iliyoambatana na upepo mkali imeezua paa za vyumba vitatu vya madarasa na nyumba mbili za walimu katika shule ya msingi Bukumi iliyopo Kata ya Bukumi.

Mvua hiyo iliyonyesha Machi 9, majira ya saa tisa usiku pia imesababisha familia tisa kukosa makazi kutokana na paa za nyumba zao kuezuliwa na upepo katika kijiji cha Bukumi na Buraga.

Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Bukumi Jumanne Chacha amesema, mbali na kuezuliwa kwa majengo ya madarasa na nyumba za walimu, mvua hiyo pia imesababisha uharibifu wa chakula, vitabu na madaftari ya wanafunzi mali zilizokuwemo kwenye ofisi na stoo ya shule hiyo.

Mwalimu William Rungongo ambaye ni mmoja wa walimu ambao nyumba zao zimeezuliwa alisema: “haikuwa hali ya kawaida kwa usiku wa leo, nimeangaika na familia yangu namshukuru Mungu nimetoka salama.”

Wakijadili kwenye kikao cha dharura cha kamati ya shule kilichowashirikisha wajumbe wa serikali ya kijiji cha Bukumi na uongozi wa kata ya Bukumi, wamekubaliana kuwatafutia walimu hao nyumba za kuishi kwa muda kijijini hapo wakati serikali ikifanya maandalizi ya kukamilisha nyumba moja ya mwalimu ambayo ipo katika hatua nzuri ya ujenzi na kujenga nyumba nyingine za walimu.

Hata hivyo, Diwani wa kata ya Bukumi John Manyama amebainisha kuwa tukio hilo ni kubwa ndani ya kata yake na atashirikiana na serikali ya kijiji na wananchi na wadau mbalimbali kufanikisha ukarabati wa miundombinu iliyoharibiwa na kuongezea kuwa, limekuwa jambo jema kwa kuwa familia za walimu wa shule yake zimetoka zikiwa salama.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi wa kijiji cha Bukumi wamesikitishwa na matukio ya namna hiyo ambayo yanaendelea kujitokeza mara kwa mara ndani ya kijiji chao na kata ya Bukumi kwa ujumla.

Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo ameahidi kuwatembelea wahanga wa tukio hilo na kutoa msaada ikibidi, huku ofisi yake ikiendelea kufuatilia kwa karibu suala hilo ambalo ni mara ya pili kwa siku za karibuni; wiki iliyopita watu watatu walifariki dunia kwenye kijiji cha Bwai Kumsoma baada ya nyumba waliyokuwa wanaishi kuanguka kufuatia mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali.