PROF. MUHONGO AWEKA WAZI MATUMIZI YA FEDHA ZA MFUKO WA JIMBO

Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo akitoa maelekezo kwa Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Musoma Charles Magoma (kushoto) wakati wa kikao cha kujadili matumizi ya fedha za mfuko wa jimbo 13, Novemba, 2017 katika kijiji cha Kabegi kata ya Ifulifu.

Na. Fedson Masawa

MBUNGE wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo ameweka wazi matumizi ya fedha za mfuko wa Jimbo la Musoma vijijini kwa kufanya kikao maalum na viongozi na wananchi wa jimbo hilo.

Kikao hicho kilichoongozwa na Prof. Muhongo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha za Mfuko wa Jimbo, kilihudhuriwa na Mkuu wa mkoa wa Mara Adamu Malima, Mkuu wa wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney, madiwani wa Musoma vijijini, viongozi mbalimbali kutoka Halmashauri ya wilaya ya Musoma, wananchi na viongozi mbalimbali wa kata na vijiji kutoka Musoma Vijijini.

Akisoma taarifa ya matumizi na mgawanyo wa fedha hizo afisa mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Joldan Hojode alisema: “kutokana na kupokea maoni mbalimbali kutoka kwa wananchi wa jimbo la Musoma vijijini na viongozi mbalimbali wa kata na vijiji walipendekeza fedha hizo zielekezwe katika kuezeka vyumba vya madarasa ambapo maoni hayo yameheshimiwa na kuifanya kamati¬† ielekeze fedha za mfuko wa jimbo kwenye uezekaji wa vyumba vya madarasa kama walivyopendekeza wananchi.”

Hata hivyo Hojode alisema, fedha hizo zitatumika kununua mabati ya kutosha kuezeka vyumba 17 vya madarasa kwani kila chumba kitapewa jumla ya mabati 54.

Kwa upande wake Prof. Muhongo amewataka madiwani kujituma na kusimamia vyema fedha hizo ili zifanye kazi iliyolengwa ikiwa ni pamoja na kufuatilia miradi yote iliyofadhiliwa na mfuko wa jimbo.

Prof. Muhongo pia amewasisitizia wananchi na viongozi kujituma katika kuongeza kasi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, kilimo cha chakula na biashara ikiwa ni pamoja na alizeti na pamba ili kuinua kiwango cha elimu, upatikanaji wa chakula pamoja na kuinua uchumi wa jimbo.

Sambamba na hayo, Prof. Muhongo alipata fursa ya kuungana na Mkuu wa mkoa wa Mara, Mkuu wa wilaya na viongozi mbalimbali kuwapa pole wananchi ambao zaidi ya nyumba 40 ziliezuliwa na kubomolewa baada ya upepo uliombatana na mvua kubwa na kusababisha baadhi ya kaya kukosa makazi katika kata ya Ifulifu kijiji cha Kabegi.

Aidha, akijitambulisha kwa wananchi wa Musoma vijijini Mkuu wa mkoa wa Mara Adamu Malima, aliwataka viongozi na wananchi kutimiza majukumu yao katika kufanya shughuli za maendeleo kuliko kusubiri kusukumwa na ngazi ya juu.

Wakishukuru kwa nyakati tofauti wananchi waliohudhuria kikao hicho wamemshukuru Prof. Muhongo na uongozi wa Mkoa na wilaya kwa uamuzi mzuri wa kugawa fedha za mfuko wa jimbo na kuridhika na mgawanyiko wa fedha hizo katika kanda zote za jimbo la Musoma vijijini.

Akifunga kikao hicho, Mwenyekiti wa kijiji cha Kabegi Charles Choto, aliwashukuru viongozi wa wilaya na mkoa kwa kuwahi kuwafikia wananchi wa kijiji chake hasa katika matukio ya kubomoka na kuezuliwa nyumba zao na akaahidi kutoa ushirikiano katika kutekeleza vyema shughuli za maendeleo.

“Nakushukuru sana Mheshimiwa DC kwa moyo wa huruma uliouonesha hasa baada ya kupata taarifa ya maafa haya kwenye kijiji changu na kufika kwa wakati. Nawashukuru Mbunge, Mkuu wa mkoa na viongozi wengine kwa kuwafikia wananchi wangu. Tutashirikiana zaidi na zaidi katika kusimamia na kutekeleza shughuli za maendeleo jimboni” alishukuru Choto.