MKUU WA WILAYA YA MUSOMA AFANYA ZIARA KUHAMASISHA MAENDELEO

Mkuu wa wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney akizungumza na viongozi mbalimbali ndani ya wilaya yake kuhusu maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na maabara unaoendelea kwa kasi.

Na. Juma Shabani

MKUU wa wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney amefanya ziara kwenye kanda ya Bukwaya na Mugango kwa ajili ya kuhamasisha shughuli za maendeleo.

Katika ziara hiyo, Dkt. Naano aliyeambatana na viongozi mbalimbali wa halmashauri, alifanya mazungumzo maalumu na viongozi wa vijiji, kata na wenyeviti wa vitongoji wa wilaya ya Musoma vijijini kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja ya kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya elimu na afya.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Musoma vijijini Charles Magoma, akifungua mkutano wa Mkuu wa wilaya na viongozi hao, alitoa taarifa ya fedha zilizotolewa na Halmashauri kwa ajili ya miradi ya ujenzi wa zahanati na vyumba vya madarasa.

“Tumetoa pesa kwa ajili ya zahanati na shule zilizokuwa zimefikia katika hatua ya upauwaji, tumetoa milioni 20 Chirorwe, milioni 20 Nyegina, milioni 15 Kigera Etuma na shule za msingi baadhi, hiyo yote ikiwa ni pesa ya halmashauri iliyokuwa imekusanya kwenye ushuru” alisema Magoma.

Mwenyekiti Magoma aliendelea kusema, ipo miradi mbalimbali iliyopo na inayotarajia kufunguliwa ambayo ikikamilika itasaidia kuongeza mapato ya halmashauri.

“Tupo katika hatua za mwisho za kujenga stendi kubwa ndani ya halmashauri hii ikiwa ni Busekera, Murangi na Mugango, nina imani kuwa hizo stendi zitakapokamilika tutakuwa tumejiongezea sehemu za ukusanyaji wa mapato” alisema.

Aidha, Magoma alisema wana mpango wa kuanzisha mwalo kwenye eneo la Nyamrinda kijiji cha Etaro kwa ajili ya kuboresha biashara ya samaki ambapo hatua hiyo itasaidia kuinua uchumi wa eneo hilo.

“Kwenye mwalo huo kutakuwa na maegesho ya maboti yanayovua samaki na sehemu ya kupaki magari yanayosimama kwa ajili ya kusubiri kusafirisha samaki kwenda kwenye maeneo mbalimbali, hivyo tutakuwa tumeongeza mapato ndani ya halmashauri yetu, halmashauri imejipanga vizuri kuhakikisha tunajenga mwalo mkubwa na wakisasa kabisa utakao kuwa na uwezo mkubwa wa kuingiza watu wengi na biashara mbalimbali”

Mwenyekiti Magoma aliwataka viongozi hao kusaidia jitihada za kusukuma gurudumu la maendeleo kwa kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato ili vijiji ambavyo havina zahanati vipate huduma hiyo kutokana na mapato hayo.

“Kuna vijiji vingi havina zahanati, hivyo ni jitihada zetu viongozi wa vijiji na kata kuhakikisha tunasimamia vizuri ukusanyaji wa mapato ili tufanye maendeleo mengi katika halmashauri yetu ikiwemo kujenga zahanati” alisisitiza Charles Magoma.

Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney alitoa shukrani zake za dhati kwa viongozi wanaomuunga mkono katika kuhakikisha wilaya hiyo inapata maendeleo.

“Nawashukuru sana wenyeviti wa vitongoji, wenyeviti wa vijiji watendaji wa vijiji na kata kwa kuonyesha moyo wa kusimamia maendeleo yetu na kuhakikisha tunapata maendeleo kwa kasi. Ndugu zangu viongozi katika halmashauri hii hatuna madarasa ya kutosha, kuna wanafunzi bado wanasomea nje wakati tuna uwezo mkubwa kabisa wa kujenga vyumba vya madarasa hata tukijiwekea malengo kwa mwaka tukiwa tunajenga vyumba viwili vya madarasa ndani ya muda mfupi tutakuwa tuna vyumba vingi na vya kutosha hivyo watoto hawatasomea nje” alisema Dkt. Naano.

Mkuu huyo wa wilaya pia alisema, ndani ya wilaya yake hakuna maabara katika shule za sekondari, jambo ambalo litaikosesha wilaya hiyo wataalamu wa sayansi kwasababu wanafunzi watashindwa kufanya vizuri masomo yao ya sayansi na kuishia mitaani.

“Vijana wengi wamekuwa wakishindwa kufanya vizuri masomo ya sayansi na kubaki kuwa mtaani bila kazi na kuzurura hovyo bila kazi, hivyo sisi wenyewe ndo inatakiwa tujenge maabara, hakuna mtu atakaye toka Kilimanjaro kuja kutujengea maabara hapa, hivyo ni juhudi zetu viongozi kuwakikisha tunawahamasisha wananchi vizuri ili kuhakikisha tunajenga maabara tena za kisasa kabisa” alisema.

Hata hivyo, Dkt. Naano alisema kuna vitu kwasasa wilaya hiyo haina tatizo navyo vikiwemo vitabu na madawati ambayo yaliwekewa mkakati maalum na mbunge wa Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo na kumaliza matatizo hayo.

“Sisi viongozi tumuunge mkono mheshimiwa mbunge katika mambo mengine na sio kila kitu kumuachie yeye na kuna viongozi baadhi naona mmesha jisahau kabisa kufanya majukumu yenu na kumtegemea mbunge kwa kila kitu, kwa maana mnaona analeta saruji, mabati na misaada mbalimbali nasema tufanye kazi wote” alisisitiza Mkuu huyo wa wilaya.

Katika kuunga mkono jitihada hizo za Prof. Muhongo, Dkt. Naano alipendekeza mchango wa Shilingi 15,000, kwa kaya ili kuhakikisha wanajenga vyumba vya madarasa na maabara katika vijiji vilivyopo wilayani humo, na kufafanua kwamba shilingi 5,000 itatolewa kwa ajili ya maabara na Shilingi 10,000 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa.

Viongozi wote walikubaliana na suala la mchango huo wa Shilingi 15,000 kwa kaya na kuahidi kuhamasisha wananchi wao kuchangia maendeleo ya elimu.

Mbali na masuala hayo ya elimu, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney aliongelea suala la uvuvi haramu na kuweka wazi kwamba wapo viongozi ambao wameshindwa kulisimamia ipasavyo kwenye maeneo yao na kuacha uvuvi huo uendelee.

“Natoa onyo tena kwa wale viongozi ambao mmeshindwa kusimamia na kukomesha suala la uvuvi haramu, nitawakamata nyie mkae jela maana haiwezekani mshindwe kudhibiti suala hilo, kuna baadhi ya maeneo uvuvi haramu umeisha kabisa, lakini bado kuna baadhi ya maeneo viongozi mnakula rushwa na kuachia wavuvi wanaendelea kufanya uvuvi haramu, nasema hakikisheni mnakomesha uvuvi haramu, wavuvi wasiotaka kufuata sheria nipeni taarifa ili tuwashughulikie” alisema.