KILIMO CHA MPUNGA CHAANZA TENA BAADA YA VIBOKO WAHARIBIFU KUUAWA

untitled

Bi. Nyanjagi Michael akiwa katika shughuli za kupanua shamba lake kwa ajili ya kilimo cha mpunga.

Na Fedson Masawa

MASHAMBA makubwa ya mpunga yaliyotelekezwa kutokana na wakulima kuhofia viboko waharibifu yameanza kulimwa katika maeneo tofauti ya kata za kandokando mwa ziwa Viktoria, jimbo la Musoma vijijini.

Hatua hiyo imekuja mwezi mmoja baada ya mtaalamu aliyesaidia kudhibiti tatizo la viboko waharibifu jimboni na kuwahakikishia wakulima kuanza kutumia mashamba yao bila hofu yoyote.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mkazi wa kijiji cha Bukumi, Nyanjagi Michael alisema wanashukuru mafanikio ya mtaalamu huyo ambaye amewasaidia kurudi kwenye mashamba yao na kuendelea na kilimo cha mpunga.

“Tunamuamini sana mtaalamu wetu, amefanya kazi nzuri kwa maana ameweza kuua viboko wawili hadi sasa hatuwaoni tena kama ilivyokuwa awali, mashamba yetu tuliyoyatelekeza tunahakikisha tutalima bila hofu yoyote” alisema Nyanjagi.

Katika hatua nyingine, mkazi mwingine wa Bukumi, Nyasami Mgono ameishukuru ofisi ya Mbunge kwa kazi nzuri na yenye mafanikio iliyofanyika ya kumpata mtaalamu ambaye amekuja jimboni humo kutatua tatizo lililoshindikana kwa miaka mingi.

“Binafsi naishukuru sana ofisi ya Mbunge wetu, kwa kazi nzuri inayofanyika kwani ni kazi yenye mafanikio. Tuliangaika kwa kipindi kirefu na sasa tumerudia kilimo cha mpunga kwenye mabonde yetu” alisema Mgono.

Kwa upande wake Nyangaso Mabure, alisema kwa mafanikio yaliyopatikana baada ya kudhibiti viboko waharibifu, wakazi wa maeneo ya kandokando mwa Ziwa Viktoria wataanza kunufaika na maeneo yao na kuwaomba viongozi wao kudhibiti kila dalili zozote zinazoashiria uvurugaji wa mazao yanayolimwa na wakulima katika maeneo hayo.

“Kwa hatua iliyofikiwa ya kudhibiti viboko waharibifu waliotusumbua kwa muda mrefu, tunaamini kila mmoja wetu kwenye eneo lake ataanza kulitumia bila kuhofu” alisema Nyangaso.

“Tunachozidi kuwaomba na kuwasihi viongozi wetu wanaohusika na hili tatizo wazidi kuwa na moyo kuendelea kudhibiti dalili zote zinazoweza kuharibu na kuvuruga mazao yetu” aliongeza na kuomba Nyangaso.

Afisa kilimo wa kijiji cha Bukumi, Alex Mihambo amethibitisha jitihada za wakulima wa kandokando mwa ziwa Viktoria hasa kijiji cha Bukumi kwa kurudisha imani yao na kuwasihi wakulima kwa kuzingatia ushauri wa wataalam.

“Wakulima hawa kweli wamerudisha imani yao baada ya kusumbuka kwa kipindi kirefu, sasa wameamua kulima mpunga katika maeneo haya. Ninachozidi kusisitiza ni kulima kilimo cha kisasa kwa kufuata ushauri wa kitaalamu” alisema na kusisitiza Alex Mihambo.