Kamati ya Mfuko wa Jimbo la Musoma Vijijini imeridhishwa na matumizi ya vifaa vilivyotolewa kupitia mfuko huo kwa mwaka wa fedha 2024/2025, baada ya kubaini kuwa kwa kiasi kikubwa vimetumika kulingana na malengo na maombi yaliyowasilishwa.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha ziara ya ukaguzi iliyochukua takribani siku tatu, Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nyegina, Thomas Nyansira, amesema kamati imefanikiwa kutembelea miradi mbalimbali ya elimu iliyonufaika na vifaa hivyo na kujiridhisha na namna vilivyotumika.
Amesema katika miradi mingi iliyotembelewa, vifaa hivyo vimetumika ipasavyo na kusaidia kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma, hususani katika sekta ya elimu, jambo ambalo linaonesha uwajibikaji mzuri kwa wahusika.
Katika hatua nyingine, Nyansira amewataka wakuu wa shule pamoja na wenyeviti wa vijiji kuhakikisha wanasimamia kwa umakini vifaa vitakavyotolewa katika mwaka wa fedha 2025/2026 ili viweze kuleta tija iliyokusudiwa kwa jamii.
Aidha, kamati hiyo imetoa shukrani kwa Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo, kwa juhudi zake za kuendelea kuwezesha upatikanaji wa fedha za mfuko huo, ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya wananchi na jamii kwa ujumla.