Halmashauri

UTANGULIZI:

Halmashauri ya Wilaya ya Musoma ilianzishwa mwaka 1984 na kuzinduliwa tarehe 29/12/1986. Aidha mwaka 2012 iliyokuwa Wilaya ya Musoma Vijijini iligawanywa na kupatikana Halmashauri ya Wilaya ya Musoma na Halmashauri ya Wilaya Butiama.

HALI YA HALMASHAURI  

Halmashauri ya Wilaya ya Musoma vijijini ni moja kati ya wilaya saba zilizopo mkoani mara, nyingine zikiwa ni wilaya ya Butiama, Serengeti, Bunda, Tarime Rorya na Musoma Mjini. Mwaka 2012 Halmashauri hii iligawanywa na kuzaa Halmashauri ya Butiama na yenyewe pia kuhamishiwa Wilaya ya Butiama kutokana na mkanganyiko huo Halmashauri ya Musoma ilitakiwa kuhama kwenda kwenye Wilaya yake mpya ya Butiama, lakini baadae iligundulika Halmashauri ya Musoma Haitakiwi kuwa Wilaya ya Butiama na hivyo kuendelea kuwa Wilaya ya Musoma mpaka hivi sasa, hivyo Mali zote zisizohamishika zitaendelea kubaki kuwa za Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.

MAHALI ILIPO NA MIPAKA YAKE

Wilaya ya Musoma Vijijini inapatikana Bara la Afrika ukandawa Afrika Masharikinchini Tanzania,Mkoa wa Mara Jimbo la Musoma vijijini.Halmashauri hii inapatikana kati ya Latitudo 1°30’ na latitudo 2°00’ Kusini mwa Ikweta na kati ya Longitudo 32°15’ na 30°15’ Mashariki mwa mstari wa Ikweta.

MIPAKA YAKE:-

Kwa upande wa Mashariki mwa jimbo la Musoma vijijini, kuna kijiji cha Kaburabura kilichopo kata ya Bugoji ambayo inapakana na kijiji cha Kangetutya kilichopo wilayani Bunda. Pia kijiji cha Kinyang’erere kilichopo kata ya Bugwema (Musoma vijijini) kinapakana na kijiji cha Karukekere kilichopo wilayani Bunda.

Kwa upande wa Kaskazini Mashariki mwa jimbo la Musoma vijijini, kijiji cha Nyasaungu kilichopo kata ya Ifulifu (Musoma vijijini) kinapakana na kijiji cha Songora katani Buruma na kijiji cha Bisumwa kata ya Bisumwa zote zikiwa katika wilaya ya Butiama. Kata ya Mugango (Musoma vijijini) pia inapakana na kijiji cha Kamgegi kilichopo wilayani Butiama.

Upande wa Kaskazini mwa jimbo la Musoma vijijini kuna kijiji cha Kurumuli kata ya Nyegina ambacho kinapakana na kata ya Buhare iliyopo Manispaa ya Musoma. Pia kijiji cha Mmaare kilichopo Kata ya Etaro (Musoma vijijini) inapakana na mtaa wa Bukanga uliopo kata ya Makoko Manispaa ya Musoma.

Hata hivyo, jimbo la Musoma vijijini limezungukwa na ziwa victoria kwa upande wa Magharibi, Kaskazini Magharibi, Kusini, Kusini Magharibi na Kusini Mashariki.

UTAWALA

Maeneo ya Kiutawala (Administrative Units – Machi 2016).Wakati Wilaya ya Musoma inagawanywa kupata Halmashauri ya Wilaya ya Butiama ilikuwa na Tarafa 3 ya Nyanja,Kiagata na Makongoro, Kata 34,Vijiji 126 na Vitongoji 564, kwa sasa Halmashauri ya Wilaya Musoma ina Tarafa 1, Kata 21 Vijiji 68 na Vitongoji 375.

Hali ya kisiasa

Hali ya kisiasa ni nzuri hakuna matukio yoyote ya migogoro ya kisiasa baina ya chama kimoja na kingine. Vipo vyama 7 vya siasa;CCM, NCCR, CHADEMA, CUF, APPT Maendeleo, ADC na ACT- Wazalendo, ambavyo kwa pamoja vina ushirikiano wa kuridhisha katika mambo mbalimbali ya kisiasa.

Hali ya Ulinzi na Usalama

Hali ya Ulinzi na Usalama katika Halmashauri ni shwari ukiacha matukio machache ya uvunjivu wa amani.

Serikali katika Wilaya ya Musoma vijijini kwa kushirikiana na wadau wengine imelipa kipaumbele Suala la Polisi jamii na ulinzi shirikishi katika kukabiliana na matukio kama ya uvunjifu wa amani kwa siku za usoni.

Aidha, kwa suala la kusalimisha silaha zinazomilikiwa kinyume cha Sheria Wilaya imewatangazia wahusika kusalimisha silaha hizo kwa ajili ya uhakiki, hata hivyo wananchi wametangaziwa kuwabaini na kuwafichua watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria na kuwaripoti haraka katika vyombo vya usalama au ngazi za uongozi.

Uongozi wa Halmashauri kwa kupitia watendaji wa vijiji, kata, vikao vya serikali ya vijiji na Mikutano Mikuu ya Vijiji imehamasisha wananchi kuachana na Imani za Kishirikina zinazosababisha mauaji ya watu hususani vikongwe na Wazee.

HALI YA WATUMISHI

Idadi ya Watumishi

Halmashauri ina jumla ya watumishi 1918 kati ya wanaohitajika 2770, kwa mchanganuo ufuatao:-

4.2.      Idadi ya Watu

Idadi ya watu kwa matokeo ya Sensa ya mwaka 2012 walikuwa 216,409 (wanaume 106,163, wanawake 110, 246) ambapo kwa matokeo ya sasa idadi ya watu inakadiriwa kuwa 227,230.

 

5.0.      HUDUMA ZA JAMII

Halmashauri ina shule za Msingi 108 ambazo zote ni za serikali, shule za Sekondari 19, hivyo sekondari 17 za serikali na 2 za binafsi. Kati ya Shule 17 za Serikali zilizo na kidato cha V na VI ni mbili ambayo ni Kasoma na Nyegina ambazo zimekwisha sajiliwa.

Halmashauri haina Hospitali ya Wilaya, kuna kituo kimoja cha Afya cha Murangi, Zahanati 27 na Ambulance zipo tano (5) kubwa moja ambayo ipo Kituo cha Afya Murangi na ndogo zipo nne katika vijiji vifuatavyo; Masinono, Kurugee, Mugango na Nyakatende.

Upande wa huduma ya maji, wananchi hujipatia maji kutoka vyanzo vifuatavyo; kwa Njia za asili, Ziwa, Visima vifupi 52, Visima virefu 34, Manteki 16 ya kuvuna maji ya mvua na Malambo 10.

5.1.      Usafirishaji na Uchukuzi:

Miundombinu ya Barabara katika Halmashuri kwa sasa ni kama ifuatavyo:

  1. Barabara za Kitaifa –                       Km 0.00
  2. Barabara za Wilaya  –                       km 103
  3. Barabara za vijiji      –                       km 250.90

Halmashauri ya Wilaya imeendelea kuifanyia matengenezo miundombinu ya barabara zake, hivyo kuimarisisha huduma ya usafiri na usafirishaji.

Mtandao wa Mawasiliano

Uwepo wa mtandao wa mawasiliano ni muhimu katika kushawishi shughuli na miradi ya maendeleo.

Kwa sasa maeneo yoteya Wilaya ya Musoma vijijini yanafikika kwa mawasiliano ya simu za mkononi. Kuwepo kwa mawasiliano kumesaidia wananchi kurahisisha kufanya shughuli zao ikiwemo kufanya mihamala ya fedha na kupata taarifa kupitia intaneti kwa urahisi. Makampuni yanayotoa huduma za simu katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ni VODACOM, TTCL, ZANTEL, TIGO AIRTEL.na HALOTEL

Nishati / Umeme

Hadi kufikia 31 Machi, 2016 msambazaji wa umeme vijijini (REA) amekamilisha kuvipatia umeme vijiji 32 kati ya 68 (Jumla ya wateja 925wameunganishiwa umeme) katika Kata 19 kati ya 21 za Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.

Aidha Wizara ya Nishati na Madini kupitia wakala wa umeme Vijijini (REA) inaendelea kukamilisha usimikaji wa nguzo na kufunga waya katika Vijiji 23 kati ya Vijiji 36 vilivyobaki.

Madini

Uchimbaji wa madini hufanywa katika kiwango cha chini kutokana na aina ya uchimbaji na vifaa duni vinavyotumika na wachimbaji wadogo wadogo. Madini yanayopatikana katika Halmashauri ya Wilaya ni dhahabu, Gemstone na Colin. Madini haya yanapatikana katika maeneo ya Ekungu, Suguti, na Seka. Aidha shughuli za uchimbaji wa dhahabu wa kati umeanza huko Kataryo. Halmashauri ya Musoma vijijini inatarajiwa kuongeza mapato yake ya ndani kutokana na tozo zitokanazo na madini haya, Kampuni ya CANTA Mine ndiyo inayojihusisha na uchimbaji huo.

Hali ya Uchumi

Inakadiriwa kuwa asilimia 90 ya wakazi wa Wilaya hii hutegemea kilimo, ufugaji, uvuvi na BiasharaKama njia ya kujipatia kipato na chakula. Kilimo katika Wilaya hii kwa kiwango kikubwa hutegemea mvua, ingawaje kuna sehemu ndogo ya kilimo cha umwagiliaji cha takribani Ha.171 kati ya Ha. 4,700 zinazofaa kwa umwagiliaji.

Maeneo ya Kataryo, Maneke, Chirorwe, Bukima, Bwaikwitururu, Masinono yameainishwa na kuandaliwa ili kutafutiwa fedha za kujengewa miundombinu/kukarabati wakati yakiendelea kutumika kwa njia za kienyeji. Mazao yanayolimwa hapa Wilayani ni Muhogo, Mahindi, Mtama, Viazi, Ufuta, Alizeti, Maharage na Pamba. Aidha Matunda na Mbogamboga hulimwa kwaajili ya Walaji wa Mjini na Vijijini.

Pato la Wilaya

Pato la Halmashauri/Wilaya kwa msimu wa mwaka 2014/2015 lilikadiriwa kuwa Tshs. 119,016,000,000 na pato la mtu/Mwananchi kwa msimu huo lilifikia Tshs. 551,000 kwa kuchukua mapato yote yalipatikana katika Wilaya kwa msimu huo.

PATO LA MWANANCHI MMOJA MMOJA (PER CAPITAL INCOME).

Hali ya pato la mwananchi mkazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma limekuwa likiongezeka mwaka hadi mwaka. Kwa msimu wa mwaka2012/2013 hadi 2014/2015 pato la mtu kwa mwaka limeongezeka kutoka wastani wa Tshs. 343,479 hadi kufikia wastani wa Tshs. 551,000 likilinganishwa na mwaka 2009/2010 hadi 2010/2011, ongezeko likiwa sawa na asilimia 60.4(%).

Katika Jitihada za kuinua pato la wananchi, Halmashauri imewahamasisha wananchi walime mazao yanayostahimili ukame, kama vile mtama, muhogo, Viazi, Dengu na alizeti.  Hata hivyo Halmashauri imejiwekea mikakati ifuatayo ili kuongeza kipato kwa wananchi wake:-

  • Kuhimiza kilimo kinachozingatia tija kati ya mazao ya chakula na biashara.
  • Kuboresha na kuendeleza kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia mabonde ya yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji kwa kujenga miundombinu ya umwagiliaji pamoja na kutumia pampu za umwagiliaji kandokando ya ziwa umbali wa mita 60.
  • Kuhimiza matumizi ya pembejeo na zana bora kwa wakulima wetu (Mf. Matumizi ya mbegu bora, Mbolea, Utumiaji wa Matrekta, Wanyamakazi, Power tiller n.k).
  • Kuendelea kuboresha sekta ya uvuvi na ufugaji nyuki ili ziwe na tija.
  • Kuhimiza uanzishaji na uendelezaji vikundi mbalimbali vya ujasiriamali ili kuongeza ajira na kipato.
  • Kuhamasisha wananchi kujiunga na SACCOS na kujiwekea akiba za kutosha zitakazowezesha kukopa na kuongeza mtaji katika shughuli zao za uzalishaji mali.
  • Kuwezesha mafunzo mbalimbali toka taasisi zinazojihusisha na Kilimo.
  • Kuanzisha na kuendeleza Mashamba darasa katika Vijiji mbalimbali kwa mazao ya Alizeti, Pamba, Mihogo, Viazi, mahindi na Mpunga.

Hali Mapato ya Ndani

Katika kipindi cha 2010 hadi 2015 wigo wa makusanyo ya ndani uliendelea kuboreshwa kutoka na kupitishwa kwa sheria kadhaa za ukusanyaji wa mapato. Aidha, hali ya makusanyo ya ushuru wa pamba haikuwa imara (stable) hivyo kushuka kutoka asilimia 3 hadi 2.

Usimamizi wa Fedha

Kumekuwepo na uimarikaji wa usimamizi wa fedha za serikali pamoja na kuboreka kwa shughuli za maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma. Katika kipindi cha mwaka 2009/2010 hadi 2013/2014 Halmashauri ya Wilaya ya Musoma imeweza kusimamia vizuri fedha zilizopatikana katika vyanzo mbalimbali na kupata hati safi kama inavyooneshwa kwa muhtasari wa hati za ukaguzi zilizotolewa kwa Halmashauri kwa kipindi cha miaka mitano.

Ushirikishaji Umma 

Nguzo na msingi mwingine wa utawala bora ni ushirikishaji wa wananchi katika kupanga, kutekeleza, usimamizi, kufuatilia na kutathmini maendeleo yao.

Katika kipindi cha kuandaa mipango ya mwaka wa fedha 2015/2016 hadi 2015/2017, Wananchi wameshirikishwa katika kuibua miradi ya vipaumbele vyao ambavyo vimewekwa katika mipango ya Maendeleo – Halmashauri ilipokea vipaumbele toka katika Kata 57 ambayo iliingizwa katika Mpango wa Halmashauri 2016/2017.

Ushirikishwaji wananchi:

Halmashauri ya Wilaya imeendelea kuhakikisha kuwa wananchi wanashirikishwa katika shughuli zote za maendeleo zinazofanyika kuanzia ngazi za Vitongoji, Vijiji, Kata na Wilaya; kupitia ushiriki katika kupanga, kuamua, kutekeleza, kusimamia na kutathmini miradi inayotekelezwa kwaajili yao.

MAENDELEO YA HUDUMA ZA KIUCHUMI NA MCHANGO WA SEKTA MBALIMBALI KATIKA KUBORESHA UCHUMI WA WILAYA

Uchumi wa wananchi wa  Wilaya ya Musoma hutegemea zaidi shughuli za kilimo, ufugaji , Biashara na uvuvi. Shughuli hizi huajiri zaidi ya asilimia 96 ya wakazi wa Wilaya hii. Shughuli za uvuvi hufanyika katika Vijiji takribani 33 vya mwambao wa ziwa Viktoria.

Shughuli za uchimbaji madini unaohusisha makampuni makubwa na wachimbaji wadogo umeanza katika vijiji vya Seka, Mabui, Suguti, Kataryo na Kigera Etuma. Biashara ndogo ndogo zinazofanywa katika miji midogo na kwenye minada na magulio pamoja madini huchangia kiais cha 4%  ya Uchumi wa Halmashauri. Kutokana na kuanza kwa uchimbaji wa kati, mchango wa sekta ya madini utaongezeka.

Sekta ya Kilimo

Eneo la kilimo

Halmashauri ya Wilaya ina jumla ya eneo lenye ukubwa wa hekta 108,675 linalifaa kwa kilimo, kati yake ni hekta 66,350 tu ndiyo zinatumika. Idadi ya kaya zote katika Halmashauri ni kaya 52,830 kati ya hizo kaya zinazotegemea kilimo ni kaya 42,264 sawa na asilimia 80 na kaya 7,566 sawa asilimia 20 zijihusishazo na Kilimo na ufugaji, hali inayosababisha Sekta ya Kilimo kuendelea kuwa ndio msingi wa uchumi unaoweza kutokomeza umasikini kutokana na kuajiri zaidi ya 80% ya wananchi.     

Hali ya Hewa:

Wilaya ya Musoma ipo katika mwinuko wa mita 1,000 hadi 1,500 kutoka usawa wa ziwa victoria, ikiwa imegawanyika katika kanda mbili za Kilimo. Ukanda wa Chini wa mwambao wa ziwa Victoria upo kati mita 1,000 hadi 1,200 ukijumuisha eneo la umbali wa km 0 – 15 kutoka katika ufukwe wa Ziwa Victoria. Ukanda wa Kati unaanzia mita 1,100 hadi mita 1,500 toka usawa wa ziwa. Aidha shughuli kuu ya wakazi wanaoishi katika maeneo haya ni uvuvi, kilimo na Ufugaji.

Umbile la ardhi katika Wilaya ni mchanganyiko wa Vilima na mabonde hasa sehemu za Kusini Mashariki na ukanda wa magharibi ambao ni mwambao wa ziwa,unaoambatana na rasi, ghuba, miteremko, tambarare, mawe yaliyojitokeza na mito inayotiririsha maji yake katika ziwa victoria.

Aina kuu za udongo zilizoko katika Wilaya ya Musoma ni (i) kichanga chenye kina kirefu (Cambic Arenosols); (ii) kichanga chenye tabaka gumu (Planosols); (iii) mfinyanzi mwekundu (Rhodic Ferralsols), (iv) mfinyanzi mweusi, unaopasuka nyakati za kiangazi (Vertisols) , (v) udongo wenye kina kifupi (Leptosols),na (vi) Udongo wa sehemu zinazotuamisha maji kwa kipindi kirefu (Graysols).

Kiasi cha mvua kwa mwaka ni kati ya mm 800 hadi 1000 kwa misimu miwili (Double Maxima) ya mvua. Mvua za msimu wa vuli huanza mwezi Oktoba hadi Desemba wakati mvua za masika huanza mwezi Machi hadi Juni. Hali ya hewa ni ya joto la kadri, lenye vipimo vya nyuzi joto kati ya nyuzi 24oC hadi 32oC; hali hii huwezesha kilimo cha Mazao aina mbalimbali kama muhogo, viazi vitamu mtama, mahindi, maharage, mpunga, uwele, pamba na alizeti. Mazao ya bustani yanayolimwa ni nyanya, kabeji, bilinganya, pilipili hoho, mchicha, vitunguu, matango, pilipili, mbuzi na spinachi katika eneo hili.

Huduma za ugani

Shughuli zinazo husika na ugani zimeimarishwa kwa kuongeza idadi ya maafisa ugani kwa ngazi za kijiji na kuwafikia wananchi kwa ukaribu zaidi ambapo wakulima wawezeshaji 60 wanafanya kazi kwa kusaidiana na maafisa ugani, kutoa mafunzo mbalimbali kwa maafisa ugani na wakulima, kurahisisha usafiri (kwa kutoa Pikipiki 9, Baiskeli 30)  kwa maafisa ugani na wakulima wawezeshaji.

Matumizi ya Zana Bora

Kiwango cha matumizi ya zana bora za kilimo katika Halmashauri ya Wilaya Musoma yako chini. Kuna Matrekta 12, Matrekta madogo (Power tiller) 3, Wakulima wadogo wanaotumia matrekta 6,492 (3%), Mikokoteni 216, Jozi za wanyama kazi 3,840, Idadi ya plau 1,280, Idadi ya wakulima wanaotumia plau 25,969 (12%) na Wakulima wanaotumia jembe la mkono 18,195 (85%).

Halmashauri imeendeleza mkakati wake wa kuinua uzalishaji mazao ya Kilimo na Biashara kwa kutumia zana bora za Kilimo kwa kuhamasisha wakulima, vikundi na watu binafsi wenye uwezo wa kununua au kukopa matrekta kwenye Mfuko wa Pembejeo wa Taifa.

Hali ya chakula Katika Halmashauri:

Mahitaji ya chakula, mahitaji ya chakula kwa wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Musomavijijini ni wastani wa tani 57,000 kwa mwaka. Kutokana na mwenendo wa uzalishaji katika kipindi cha mwaka 2011/2012 hadi 2015/2016 kiliambatana na upungufu wa mara kwa mara wa chakula, pengo ambalo huwa linazibwa kwa chakula cha Msaada wa njaa ambacho hutolewa na Kitengo cha Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu na wafanyabiashara waliohamasishwa kuendelea kununua chakula nje ya wilaya na kuuzia wananchi katika maeneo yale yanayoonekana kuwa na uhaba mkubwa. Katika msimu wa vuli kwa mwaka huu 2015/2016 uzalishaji wa nafaka na mikunde ulifikia tani 31,228.9, na kufanya kaya nyingi kuweza kujitosheleza kwa chakula. Utoshelevu huu utaendelea pale mavuno ya msimu wa msaika yatakapokuwa mazuri. Hivyo wananchi wanashauriwa waendelee kutumia vizuri mvua zinazoendelea kunyesha kwa kupanda mazao, pia wasiuze chakula watachovuna kwa ajili ya kujipatia fedha.

Miundombinu ya Mifugo

Halmashauri ya Wilaya ina jumla ya majosho 11 yanayofanyakazi.

 SEKTA YA UVUVI

Halmashauri ya Wilaya iko katika mwambao wa Ziwa Victoria, uvuvi ni mojawapo wa shughuli muhimu ya kiuchumi (huchangia wastani wa 30% ya pato la wilaya) kwa wakazi wake hasa waishio kando kando ya ziwa. Wakazi katika vijiji 33 na visiwa 6 wanategemea uvuvi kama shughuli kuu katika maisha yao ya kila siku. Takwimu za mwaka 2014 zinaonesha kuporomoka kwa shughuli za sekta ya uvuvi ukilinganisha na takwimu ya sensa ya uvuvi ya mwaka 2012.

Uzalishaji wa Mazao ya Samaki:

Wastani wa uzalishaji wa samaki ni tani 12,082.41 zenye thamani ya shilingi bilioni   33,754,393,170 Kwa mwaka. Kwa kipindi cha mwaka 2010/11 – 2015/16 mwenendo wa uzalishaji na Makusanyo ya mapato [mauzo ya samaki waliovuliwa (Sangara, Sato, Dagaa).

SEKTA YA ARDHI NA MALIASILI

Ardhi:

Halmashauri kwa kutambua umuhimu wa rasilimali ardhi kiuchumi na kijamii, uwekezaji umejikita katika kuona kuwa utekelezaji wake unazingatia Mipango ya Matumizi bora ya ardhi. Halmashauri imeendeleza jitihada za Uandaaji wa Mipango Miji na Upimaji Viwanja, Mipango ya Uwekezaji Mkubwa/Mdogo na Uwekezaji katika uchimbaji wa madini na Hoteli.

Matumizi bora ya ardhi

Lengo la Halmashauri ya Wilaya ya Musoma vijini limekuwa ni kuvishirikisha vijiji kubainisha kwa uelewa wao ukubwa wa ardhi iliyopo na matumizi,hivyo fomu maalumu imeandaliwa na kuisambaza kwa watendaji wote wa vijiji na kata itakayosaidia kupata taarifa na Takwimu za awali zitakazowezesha Halmashuri baadaye kuvisaidia vijiji kuandaa Mipango ya muda mrefu ya matumizi bora ya ardhi ambao utaainisha ardhi ya makundi ya wakulima na wafugaji ikianisha na matumizi mengine, ambayo yatakuwa yamezingatia;

  • Kuilinda kutokana na ujenzi holela na wakati huo mipango madhubuti ya kutatua migogoro kati ya makundi ya watumiaji ardhi wakulima, wafugaji na wafanya biashara itakuwa bayana na hatimaye iweze kutumika katika mipango ya kiuchumi endelevu.
  • kwa upande mwingine Halmshauri kuendelea kutekeleza mpango wa matumizi bora ya ardhi ya kina katika kijiji cha Suguti kama kijiji cha mafunzo na vijiji vingine vinavyofuata katika mpango huu ni Chirorwe na Wanyere kwa kadri ya uwezo na upatikanaji wa fedha.

Misitu

Halmashauri ina hifadhi moja ya Suguti iliyoandikwa katika gazeti la Serikali, yenye hekta 281.9. Ukataji wa miti umeendelea kuwa tatizo kuu linaloathiri Hifadhi ya misitu na mazingira kutokana na kuwepo kwa soko la bidhaalitokanalo na mazao ya misitu kutoka wakazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mji wa Musoma. Wakazi hawa wanategemea matumizi ya nishati ya mkaa na kuni ambayo hupatikana kutoka maeneo ya Halmashauri za Wilaya jirani, hali ambayo huchangia ukataji holela miti.

Katika kukabiliana na tatizo hili Halmashauri ya Wilaya imehamasisha jamii kupanda miti zaidi kupitia Kampeni ya upandaji miti 1,500,000 kila mwaka na kuhifadhi maeneo yaliyoharibika kwa kukatwa miti. Aidha, matumizi ya sheria zilizopo ili kudhibiti wahalifu hao na kutoa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa kutunza mazingira na madhara ya kukata miti hovyo vimeenezwa.

Uhifadhi wa uoto wa asili na upandaji wa miti:

Halmashauri imeendeleza jitihada za kuishirikisha jamii katika mkakati wa uhifadhi wa uoto wa asili na upandaji miti kwa kuweka mpango shirikishi wa hifadhi ya msitu wa Suguti wenye jumla ya hekari 281.9 kadhalika misitu ya mtiro na Mugango iliyoko katika kata za Bukumi na Mugango inaandaliwa mipango ya kuhifadhiwa kwa mwaka huu  wa fedha (2014/15).

Katika Kipindi cha mwaka 2005/06 – 2014/15, jumla ya miche ya miti 12,424,298 imeoteshwa na kupandwa na wadau wa maendeleo ikiwa ni pamoja na Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGO’s), Taasisi za Umma na Watu binafsi kama ilivyo agizo la serikali.

Ufugaji Nyuki

Shughuli za ufugaji nyuki ni miongoni mwa mazao mapya ambayo Halmashauri inaendelea kuhamasisha wananchi katika vijiji vyote wajitokeze na kujihusisha na ufugaji nyuki ili kujiongezea kipato. Kutokana na jitihada hizo hadi sasa;

(a) Vikundi 2 vinavyojihusisha na ufugaji nyuki vyenye jumla ya mizinga 6 katika kijiji cha Chirorwe, vimeanzishwa.

(b) Halmashauri ilitenga fedha T.shs.7, 500,000 kwenye bajeti ya mwaka 2013/14 kwa ajili ya kutengeneza mizinga 100 katika kijiji cha Chitare kata ya Makojo.

(c) Mkutano wa hamasa ya kuamasha ari ya ufugaji nyuki ilifanyika katika vijiji vya Chirorwe, Chitare na Butata ambapo;

–        Wanakikundi 15 walipata mafunzo ya stadi za ufugaji bora wa nyuki na utengenezaji wa mizinga.

–        Mizinga 5 ya nyuki ilitengenezwa na kikundi cha Butata pia wametenga msitu kwa ajili ya ufugaji nyuki, aidha kikundi Chirorwe wametengeneza mitatu (3) ya kisasa.

Barabara

  • Halmashauri ya wilaya ya Musoma ina mtandao wa barabara wa jumla ya km 532.303. Hali ya barabara katika Halmashauri ya wilaya ni ya kuridhisha; karibu zote zinapitika wakati wote wa masika na kiangazi, hii ni kutokana na Halmashuri kuendelea kuifanyia matengenezo miundombinu ya barabara zake zote hivyo kuwa kiungo na kichocheo kikubwa cha kiuchumi na mawasiliano kutokana na kurahisisha huduma ya usafiri na usafirishaji wa bidhaa na mazao ya wakulima kuyafikia masoko kwa urahisi. Hali ya Mgawanyiko wa barabara katika Halmashauri ni kama inavyoonyesha hapa chini:
  • Barabara za Kitaifa          Km 0.00
  • Barabara za Wilaya          Km 104.243
  • Barabara za Wilaya         Km 166.16
  • Barabara za vijiji               Km 261.9

Jumla ya Barabara            Km 532.30

Barabara hizo zimeendelea kufanyiwa matengenezo kila mwaka kwa awamu ili ziweze kupitika kwa urahisi na kurahisisha usafiri na usafirishaji.

Sekta ya Maji

Kwa kutambua umuhimu wa sekta ya Maji kwa maendeleo ya Kiuchumi, kijamii na hifadhi ya mazingira Halmashuri kuendeleza Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji ili kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama kufikia asilimia 65 vijijini na  asilimia 75 mjini ifikapo mwaka 2015.

Halmashauri ya wilaya imeendeleza jitihada za utoaji wa huduma ya Maji kwa kuzingatia sera ya upatikanaji wa huduma hiyo katika umbali usiozidi mita 400 ambao kwa sasa ni chini ya asilimia 20 kwa wakazi wa mijini na asilimia 10 kwa wakazi wa vijijini. Kutokana nautekelezaji wa miradi ya Maji bomba na uchimbaji wa visima virefu unaoendelea ikikamilika itahudumia zaidi ya watu 60,000, hivyo kuongeza watu wanaopata maji safi na salama kutoka 47.54% hadi 50% ifikapo Juni 2015 kwa muhtasari kama ifuatavyo:

  • Ujenzi wa visima virefu na vifupi umeongezeka toka visima 50 mwaka 2010 hadi visima114 mwaka 2014 likiwa ongezeko la visima 64 sawa na asilimia 128.
  • Ujenzi wa matenki ya kuvuna maji ya mvua yameongezeka kutoka matenki 36 mwaka 2010 hadi matenki 73 mwaka 2014 likiwa ni ongezeko la matenki 37 sawa na asilimia 103.
  • Miradi ya maji bomba imeongezeka kutoka vituo vya kutekea maji 21 mwaka 2005 hadi vituo 89 mwaka 2014 sawa na asilimia 323.8.
  • Malambo/ Mabwawa yameongezeka kutoka 6 mwaka 2010 hadi malambo/mabwawa 7 mwaka 2014 sawa na asilimia 17.
  • Jumuiya za Watumiaji maji zimeongezeka kutoka jumuiya 6 mwaka 2010 hadi 14  mwaka 2014 sawa na asilimia 133.
  • Mifuko ya Maji Iliyopo imeongezeka kutoka TSh.1,980,000 mwaka 2010 hadi TSh. 5,800,000 mwaka 2014 sawa na asilimia 382. 16.0.

SEKTA YA ELIMU

Elimu ya msingi:

Halmashauri ya wilaya Musoma ina jumla ya shule za Awali 108 na Msingi 111, zenye jumla ya wanafunzi 65,864 na walimu 1,038 sawa na asilimia 29 ya mahitaji.

Elimu ya sekondari:

(a)   Idadi ya shule na uwiano wa Walimu kimasomo.Katika Halmashauri ya wilaya Musoma zipo Shule za Sekondari 19 (shule 1 ni mchanganyiko wa “O” na “A” Level), shule 17 ni za Serikali na shule 2 za binafsi zinazomilikiwa na mashirika ya dini. Aidha, wapo wanafunzi 7,189 na walimu 339 ikiwa sawa na asilimia 87 ya mahitaji.