WAKULIMA MASHUHURI WA ALIZETI WAJENGA KIWANDA KIDOGO CHA KUSINDIKA MBEGU ZA ALIZETI

Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo akiwa ndani ya kiwanda kidogo cha kusindika mbegu za alizeti. Kiwanda hicho kitakachofunguliwa mwezi huu kinajengwa Kijijini Masinono, Kata ya Bugwema.

Ijumaa, 9.9.2022, Kikundi cha Changamkeni cha Kijijini Masinono, Kata ya Bugwema kimekamilisha malipo ya kufungiwa umeme kwenye KIWANDA chao cha ALIZETI kinachojengwa Kijijini Masinono. Mbunge wa Jimbo nae amechangia gharama za kufungiwa umeme kwenye kiwanda hicho.

UNUNUZI WA MASHINE YA KUKAMUA MBEGU ZA ALIZETI

*Mwaka 2020, Shirika la SHIMAKIUMU linalojishughulisha na Kilimo na Ufugaji ndani ya Wilaya yetu, lilipatia Kikundi cha Changamkeni mashine ya kukamua mbegu za alizeti.

*Mashine hiyo ina thamani ya Tsh Milioni 35 (Tshs 35m) na uwezo wa kukamua mbegu za alizeti kwa kiasi cha magunia 40 kwa siku.

Shukrani za dhati zinatolewa kwa SHIMAKIUMU kwa ufadhili huo utakaofaidisha Wana Kikundi cha Changamkeni, na wakulima wengine wa alizeti ndani ya Bonde la Bugwema na kwingineko Mkoani Mara.

KILIMO CHA ALIZETI MUSOMA VIJIJINI

Mbunge Jimbo la Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo alianza kampeni ya kushawishi uanzishwaji wa kilimo cha alizeti Jimboni mwao Mwaka 2016, na kwa misimu mitatu mfululizo (ya kilimo) aligawa bure mbegu za alizeti kiasi cha TANI 9.66. Msimu wa Mwaka 2018/2019, Wizara ya Kilimo ilichangia TANI 10.

BUGWEMA YAONGOZA KWENYE KILIMO CHA ALIZETI

Wakulima ndani ya Bonde la Bugwema ndio wanaongoza kwa kilimo cha zao la alizeti ndani ya Mkoa wa Mara.

Kikundi cha Changamkeni kinakusudia kulima Ekari 500 za alizeti ndani ya Bonde la Bugwema.

Mazao mengine yanayolimwa kwa wingi na Wakulima wa ndani ya Bonde la Bugwema ni: mahindi, mpunga, dengu na pamba.

Wakulima wa Bugwema wanasubiri kwa hamu kubwa Mradi kabambe wa umwagiliaji ndani ya Bonde la Bugwema. Mradi huo utaanza kwa ufadhili ya Serikali yetu.

 

Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Musoma Vijijini
www.musomavijijini.or.tz

Tarehe:
Ijumaa, 9.9.2022