
Jimbo la Musoma Vijijini lenye jumla ya Kata 21, lina Kata 18 zilizoko pembezoni mwa Ziwa Victoria. Kwa hiyo, uvuvi ni kazi inayoajiri watu wengi wa Jimboni mwetu.
Wataalamu wa uvuvi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, wakiwemo wa TAFIRI, walishirikiana na NEMC kubaini maeneo mazuri yanayokidhi vigezo vya kufanya uvuvi wa vizimba ndani ya Jimbo letu.
Mbali ya mikopo nafuu iliyotelewa na Serikali yetu kwenye uvuvi wa vizimba, Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo anaendelea kuwashawishi wavuvi wa Jimboni mwetu kwenda Benki za CRDB na NMB kuchukua mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya uvuvi wa vizimba. Mbunge huyo ameishawasiliana na Benki hizo mbili kuhusu mikopo hiyo.
Matunda mazuri yaanza kuonekana:
Wavuvi wa Jimbo la Musoma Vijijini wameanza kupata matunda mazuri kutokana na uvuvi wa samaki kwa kutumia vizimba.
Mvuvi mmoja (pichani) wa Kijijini Kigera, Kitongoji cha Kurukiri anavuna samaki takribani Tani 40 kutoka kwenye vizimba vyake 4 vyenye upenyo wa mita 10.
Masoko ya samaki wanaovunwa kutoka kwenye vizimba yapo, ambayo ni ya walaji na viwanda vya minofu ya samaki. Bei inaendana na ukubwa na uzito wa samaki, na kwa sasa ni kati ya Shilingi 7,000 na 10,000 kwa kilo moja.
Picha 2 zilizoambatanishwa hapa:
*Kizimba cha Ziwani Kurukiri, Kijijini Kigera, Kata ya Nyakatende
*Samaki walivuliwa leo wanaouzwa Shilingi 8,500 kwa kilo.
SHUKRANI:
Wavuvi na wananchi wa Jimbo la Musoma Vijijini wanaendelea kutoa shukrani nyingi kwa Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuonyesha njia, kwa vitendo, ya uwekezaji mkubwa kwenye uvuvi wa vizimba nchini mwetu - ahsante sana!
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Musoma Vijijini
www.musomavijijini.or.tz
P.O.Box 6
Musoma
Tarehe:
Jumapili, 1 Juni 2025